Alhamisi, 18 Februari 2021

JAJI MKUU WA TANZANIA AWAAPISHA MAHAKIMU WAKAZI WAPYA 71

·       Amshukuru Rais Magufuli kwa kibali cha ajira ya Mahakimu hao

Na Mary Gwera, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaapisha Mahakimu Wakazi wapya 71 huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa kibali maalum cha kuajiri jumla ya Mahakimu 100 ili kuongeza nguvu kazi katika huduma ya utoaji haki nchini.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha rasmi Mahakimu hao leo Februari 18, 2021 katika Viwanja vya Karimjee-Dar es Salaam, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa kibali hicho kilichotolewa na Mhe. Rais ni mfano mzuri wa uwezeshaji ambao Mhimili wa Serikali umetoa kwa Mahakama hasa katika kipindi ambacho ajira katika Taasisi za Umma ni chache.

 “Naomba kutoa shukrani maalum kwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kibali maalum kwa Mahakama iajiri Mahakimu 100. Alitoa kibali hicho siku ya sheria 2020 na kakumbushia tena siku ya sharia yam waka huu 2021,” alieleza Mhe. Jaji Prof. Juma.

Aidha, Mhe. Jaji Mkuu aliwapongeza Mahakimu hao wapya kwa kupata nafasi adhimu ya kuwa Mahakimu Wakazi na kuongeza kuwa ni uthibitisho tosha ya kuwa wameaminiwa na Mahakama kwa kushika nafasi hiyo muhimu katika Mhimili wa Dola wa kutoa haki.

Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kwa kuwataka kutekeleza majukumu yao ya utoaji haki hususani uandishi sahihi wa hukumu kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa ili kutoa haki bila vikwazo vyovyote.

“Kazi yenu kubwa ni kutoa maamuzi, au kuandika hukumu rasmi ambayo ni sehemu ya kumbukumbu ya kudumu ya Mahakama kuhusu shauri lililoletwa Mahakamani ili litolewe uamuzi. Hukumu ni uamuzi ambao utabaki kuwepo kwa miaka mingi ijayo itaonyesha namna ulivyoshughulikia huo mgogoro, ushahidi ulivyoletwa, na namna ulivyochambua vifungu vya sheria mbali mbali, kuvilinganisha na ushahidi wa pande zinazobishana, na kisha kutoa uamuzi wako,” alifafanua Mhe. Jaji Mkuu.

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Mkuu aliwataka Mahakimu hao kushirikiana na Wadau ikiwemo jeshi la polisi ili kuweza kusikiliza mashauri ya jinai ipasavyo, huku akieleza kuwa ushiriki wa ofisi ya huduma kwa jamii umenisaidia sana katika kupunguza ile haja ya kuwapeleka watu jela katika makosa madogo madogo. 

“Shirikianeni pia na Ofisi za watendaji kata kwa kuwa wanasaidia katika kufanikisha dhamana kwa washtakiwa, pia Ustawi wa Jamii katika mashauri yanayohusu utelekezwaji wa watoto wamekuwa msaada mkubwa. Hii imenijengea kuthamini mchango wa kila mdau katika utoaji haki ili kufanikisha majukumu yangu,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.

Awali akimkaribisha Mhe. Jaji Mkuu, Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma alisema kuwa idadi hiyo ya Mahakimu 71 inajumuisha wanawake 38 na wanaume 33 ambao ni miongoni mwa Mahakimu 142 waliosailiwa Septemba 14 hadi 26, 2020.

Mhe. Chuma alisema kuwa kundi la pili la Mahakimu wengine 71 lenye wanawake 37 na wanaume 34 wataapishwa na Mhe. Jaji Mkuu Februari 26 mwaka huu.

“Idadi tajwa inaonyesha ongezeko la Mahakimu wanawake katika Mhimili wa Mahakama nap engine ndio wakati wao wa kuonyesha umahili wao,” alieleza Mhe. Chuma.

Baada ya uapisho Mahakimu wote watakwenda katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto kuhudhuria mafunzo ya kuwajengea uwezo katika utendaji kazi wao.

Pichani ni Waheshimiwa Mahakimu Wakazi wapya wakila kiapo mbele ya Mhe. Jaji Mkuu (hayupo pichani). Jumla ya Mahakimu Wakazi wapya 71 wamekula kiapo hicho mapema leo Februari 18, 2021 katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.


Waheshimiwa Mahakimu wakitoa heshima mbele ya Mhe. Jaji Mkuu mara baada ya kuapishwa rasmi.


Waheshimiwa Mahakimu wakitia saini katika hati za viapo mara baada ya kuapishwa rasmi na Mhe. Jaji Mkuu.

Mhe. Jaji Mkuu akizungumza na Waheshimiwa Mahakimu wapya mara baada ya kuwaapisha.




Picha mbalimbali za Wahe. Wakifuatilia hotuba ya Mhe. Jaji Mkuu (hayupo pichani).

Mhe. Jaji Mkuu akiwaonyesha Mahakimu wapya moja ya miongozo ya Mahakama ambayo wanatakiwa kuisoma na kuifuata katika utendaji kazi wao.

Mhe. Jaji Mkuu akiwa katika meza kuu, pamoja naye ni Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (wa pili kushoto), wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Lameck Mlacha, wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru na wa kwanza kulia ni Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania.

Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akizungumza jambo katika hafla fupi ya uapisho iliyofanyika Karimjee-Dar es Salaam.

Msajili-Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt akizungumza jambo katika hafla hiyo.

(Picha na Mary Gwera, Mahakama)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni