Na Lydia Churi-Mahakama, Arusha
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
amewaomba wajumbe wa kamati za Maadili za Mkoa na Wilaya zilizopo mkoani Arusha
kufuatilia kwa karibu maboresho yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania ili waweze
kuwaelimisha wananchi.
Jaji Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi
wa Mahakama ameyasema hayo alipokuwa akifungua kikao kati ya Tume hiyo na wajumbe
wa Kamati za Maadili za Mkoa wa Arusha pamoja na wilaya zake kilichofanyika
katika ukumbi wa Hazina Ndogo mjini humo.
“Mahakama imeboresha mambo mengi ambayo wananchi walio
wengi hawajapata fursa ya kuwafahamu hivyo mkiwa karibu na Mahakama mtafahamu
mengi na kuwaelimisha wananchi”, alisema Jaji Mkuu.
Aliwataka wajumbe wa Kamati za Maadili za mkoa huo na
wilaya zake kusoma taarifa mbalimbali zinazohusu maboresho ya Mahakama kupitia
machapisho Tovuti ya Mhimili huo pamoja na machapisho mbalimbali yanayotolewa
kwa lengo la kutoa elimu ili kuwaongezea ufahamu zaidi wa shughuli za Mahakama
hatua itakayowasaidia kutekeleza wajibu wao kwa urahisi na ufasaha.
“Wananchi wengi hawafahamu majukumu ya Tume pamoja na
kamati zake na wakati mwingine hujikuta wakiwasilisha malalamiko yanayotakiwa
kushughulikiwa na katika mfumo wa kimahakama hivyo wajumbe mkifahamu mipaka ya
kazi zenu mtakuwa kwenye nafasi nzuri ya
kuwaelimisha waelewe na kutofautisha masuala ya kinidhamu nay a kimahakama”,
alisisitiza.
Alisema Mahakama imeandaa miongozi kadhaa kwa lugha ya
Kiswahili itakayosaidia katika utekelezaji wa majukumu yake, baadhi ya miongozo
hiyo ni mwongozo unaohusu masuala ya Dhamana,
wajibu wa Madalali, Utekelezaji wa amri za Mahakama pamoja na ule wa Watumiaji
wa huduma za Mahakama.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Iddi
Hassan Kimanta amesema mkoa amewashauri wajumbe wa Kamati za Maadili za wilaya
mkoani humo kuhakikisha wanajisomea nyaraka mbalimbali za Mahakama zinazohusu
majukumu ya kamati zao ili wawe na uelewa mpana na kuwaeleimisha wananchi
majukumu ya kamati hizo na namna bora ya kuwasilisha malalamiko yao.
Awali, akizungumza na Jaji Mkuu alipotembelewa na
Kiongozi huyo wa Mhimili wa Mahakama ofisini kwake, Mkuu wa mkoa wa Arusha alisema
kuwa migogoro ya kazi imeongezeka mkoani
humo na imetokana na athari za ugonjwa wa Covid 19 ambao kwa kiasi kikubwa
umeathiri sekta ya Utalii.
Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania ambaye pia ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama amesema Mahakama
inahuisha Mpango wa Ujenzi na Ukarabati wa majengo yake ili kuweza kuanza ujenzi
kwenye maeneo yenye changamoto kubwa zaidi ya miundombinu ya majengo.
Alisema Mahakama imekamilisha ujenzi wa miradi ya majengo
ya Mahakama katika maeneo ya Longido na Ngorongoro na itatoa kipaumbele kwa
mkoa huo kutokana na changamoto zilizopo.
Alisema zaidi ya majengo 10 ya Mahakama mkoani huo yanahitaji
kujengwa na mengine kufanyiwa ukarabati ili kupunguza gharama za uendeshaji
kwani baadhi ya maeneo wanachi wanalazimika kufuata huduma hizo kwa umbali
mrefu.
Naye Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama,
Bibi. Enziel Mtei amewashauri wajumbe wa kamati za Maadili kutumia elimu
waliyoipata kuhusu uendeshaji wa kamati hizo kuwaelimisha wananchi.
Alitoa wito kwa wajumbe hao kutoa kipaumbele katika
suala zima la uendeshaji wa kamati hizo kwa kutenga bajeti kwa ajili ya
kuendesha kamati za Maadili kwenye maeneo yao.
Tume ya Utumishi wa Mahakama inafanya ziara katika
Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara kwa lengo la kuitangaza na kutoa elimu
kwa wadau wa Mahakama wakiwemo wajumbe wa kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya zinazowajumuisha
wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya.
Tume ya Utumishi ya Mahakama imeundwa kwa mujibu wa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 113 kwa lengo la kusimamia
mambo muhimu yanayohusu Mhimili wa Mahakama. Wajumbe wa Tume hiyo ni pamoja na
Jaji Mkuu wa Tanzania (Mwenyekiti), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji moja wa Mahakama
ya Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, na
wajumbe wengine wawili wanaoteuliwa na Rais.
Baadhi ya kazi
za Tume hiyo ni pamoja na kumshauri Mhe. Rais katika uteuzi wa Majaji wa
Mahakama Kuu, kumshauri Rais kuhusu masuala ya nidhamu, mishahara na maslahi ya
Majaji, na kushauri kuhusu ajira za Mahakimu na kusimamia nidhamu yao.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza wakati alipomtembelea Mkuu wa Mkoa wa Arusha ofisini kwake. Kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Gerald Ndika na Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa ArushaMhe. Iddi Hassan Kimanta.
Mkuu wa Mkoa wa ArushaMhe. Iddi Hassan Kimanta akizungumza.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro akizungumza wakati wa Mkutano huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni