Ijumaa, 21 Mei 2021

JAJI MKUU PROF JUMA AZINDUA MPANGO MKAKATI MPYA WA MAHAKAMA

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amezindua rasmi Mpango Mkakati mpya wa Mahakama ya Tanzania wa miaka mitano (5) (2020/2021-2024/2025) ambao utatumika kama dira ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Mahakama ikiwa ni pamoja na kuleta maboresho ya huduma ya utoaji haki kwa wananchi.

Hafla fupi ya uzinduzi wa Mpango huo imefanyika leo Mei 21, 2021 katika Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama kilichokuwa kikifanyika katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.

Akitoa neno la utangulizi kabla ya uzinduzi rasmi, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru alisema kuwa lengo la kuwa na Mpango huo ni kuhakikisha kuwa Mahakama inafikia malengo ambayo imejiwekea katika suala zima la utoaji haki kwa wananchi.

“Huu ni mpango mkakati wa pili, mpango huu umelenga kuendeleza mazuri yote ya mpango wa kwanza, hivyo ni rai yangu kwa watumishi wa Mahakama na wadau kushirikiana kwa pamoja kama ilivyokuwa katika utekelezaji wa mpango wa kwanza ili kuweza kutekeleza ipasavyo azma yetu ya maboresho ya utoaji huduma bora kwa wananchi,” alisema Bw. Kabunduguru.

Aidha, Mtendaji Mkuu alisema kuwa kumekuwa na mafanikio katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa awamu ya kwanza wa mwaka 2015/2016-2019/2020 na hivyo kuwapongeza watumishi kwa utekelezaji na kuwataka kuendeleza ari hiyo ya ufanyaji kazi kwa manufaa ya Mahakama na wananchi kwa ujumla.

Kwa upande mwingine, Bw. Kabunduguru alieleza kuwa katika Mpango huu mpya utakuwa na nguzo kuu tatu (3) kama ilivyokuwa katika mpango wa kwanza ambazo ni Utawala, Uwajibikaji na Usimamizi wa Rasilimali, Upatikanaji wa Haki kwa wakati na Kurejesha Imani ya Wananchi na Ushirikishwaji wa Wadau.

Aliongeza kuwa Mpango Mkakati huu una Maeneo ya Matokeo (Key Result Area) saba (7), Malengo ya Kimkakati (Strategic Objectives) 17 na Viashiria vya matokeo (Key Performance Indicators) 58.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Mapngo Mkakati mpya wa Mahakama wa miaka mitano (5) (2020/2021-2024/2025), wanaoshuhudia wa pili kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, wa pili kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru, wa kwanza kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na wa kwanza kushoto ni Mhe. Julius Kalolo, Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Wakionyesha nakala za Mpango Mkakati mpya uliozinduliwa rasmi na Mhe. Jaji Mkuu.
Wakiwa na nyuso za furaha mara baada ya uzinduzi rasmi wa Mpango Mkakati mpya wa Mahakama.
Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia tukio la uzinduzi rasmi wa Mpango Mkakati mpya wa miaka mitano (5) wa Mahakama ya Tanzania 
(2020/2021-2024/2025).

(Picha na Mary Gwera-Mahakama)




 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni