Alhamisi, 22 Julai 2021

HUDUMA ZA MAHAKAMA YA MWANZO SHANWE KATAVI ZAREJEA

Na Mayanga Someke- Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga

Shughuli za utoaji huduma za Mahakama katika Mahakama ya Mwanzo Shanwe iliyopo Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi zilizositishwa kwa muda mrefu zimerejea huku Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Danstan Ndunguru akitoa rai kwa Mahakama hiyo kushirikiana na wadau ili kutoa haki kwa wakati.

Jengo la Mahakama ya Mwanzo Shanwe lilijengwa mwaka 1952 ambapo huduma za kimahakama ziliendelea kutolewa hadi mwaka 1980 zilipositishwa baada ya kukosa watumishi na hivyo huduma za Mahakama ya mwanzo zikawa zinatolewa Mahakama ya mwanzo Mpanda Mjini.

Akizungumza na wananchi pamoja na Watumishi wa Mahakama wakati wa uzinduzi rasmi wa huduma za Mahakama hiyo, Mhe. Jaji Mfawidhi huyo alisema ni muhimu kwa Watumishi wa Mahakama hiyo kushirikiana na wadau wengine ambao wanamchango mkubwa katika shughuli za kimahakama katika huduma ya utoaji haki kwa wananchi.

“Mfano tunaweza kuwa tunalalamika kesi inachelewa Mahakamani,tumegawanyika kila mmoja ana sehemu yake. Polisi ana wajibu wa kukamata, kupeleleza na kuleta ushahidi Mahakamani, Ofisi ya Mashtaka kazi yao ni kuendesha shitaka, katika mazingira hayo mmoja akizembea athari zinakuwa kwa yule mtu ambaye ana shauri na atalalamika shauri lake limecheleweshwa, hivyo kila mdau katika mfumo wa utoaji haki lazima awajibike,” alisema Mhe.Jaji Ndunguru.

Aliongeza kuwa katika kuhakikisha kwamba huduma za kimahakama zinafikika kwa urahisi lakini pia kwa wakati unaotakiwa. ‘Hatutarajii kuona mwananchi anatembea kutwa nzima kwenda Mahakamani na anafika muda wa kazi umeisha na kesi imefutwa kwasababu tu anatoka mbali kwahiyo ndo maana tunajitahidi kuhakikisha tunasogeza huduma karibu na wananchi.”

Hali kadhalika, Mhe. Jaji Ndunguru aliwashukuru Wadau wa Mahakama kwa kuchangia na kufanikisha ukarabati wa jengo hilo hali iliyowezesha shughuli za Mahakama hiyo kurejea.

Aidha, alitoa rai pia kwa Watumishi wa Mahakama hiyo kubadili mienendo na tabia zinazokiuka miiko na maadili ya kazi na Utumishi wa Umma ili waweze kutoa huduma kwa wananchi kwa ubora unaostahili.

Kwa upande wa Wananchi wa kata hiyo, Mhe Jaji Mfawidhi aliwasisitiza kutokuwa na mtazamo hasi kwa Mahakama kwani Mahakama haipo kwa ajili ya kufunga tu. 

Mahakama ya Mwanzo Shanwe ni moja kati ya Mahakama kongwe nchini na ni kati ya Mahakama za awali kujengwa katika mkoa wa Katavi. Huduma za kimahakama katika kata ya Shanwe zilianza kabla ya uhuru mwaka 1926 ikiwa ni Baraza na wakati huo Watemi ndio walikuwa wanaendesha mashauri.

Muonekano wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Shanwe likiwa tayari kwa kurejesha huduma za Mahakama.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Mhe.Danstan Ndunguru akifuatilia taarifa fupi ya ukarabati wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Shanwe, kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Mhe William Mutaki na Kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Mhe.Danstan Ndunguru akikata utepe kuashiria urejeshwaji wa huduma za Mahakama katika Mahakama ya mwanzo Shanwe-Katavi.
Watumishi wa Mahakama ya Hakimu mkazi mkazi Katavi na wilaya zake  Wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mhe Jaji Mfawidhi na viongozi wengine wa Mahakama-Kanda ya Sumbawanga.

Picha ya pamoja na wananchi wa Kata ya Shanwe.

 








 





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni