Jumanne, 26 Oktoba 2021

WATUMISHI WA MAHAKAMA WAPONGEZWA

Na Mary Gwera na Faustine Kapama, Mahakama-Bunda

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewapongeza watumishi wote wa Mahakama nchini kwa kutekeleza kikamilifu Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (5) wa 2015/2016-2019/2020 uliomalizika mwaka uliopita uliolenga kuboresha huduma za utoaji haki kwa wananchi.

Akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi, Kanda ya Musoma iliyoanza tarehe 26 Machi, 2021, Mhe. Prof. Juma alisema kuwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania wametekeleza kwa ufanisi mkubwa Mpango Mkakati huo.

“Kwa muda wa miaka mitano tumekuwa tukitekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano na tumetekeleza kwa ufanisi mkubwa na Mpango wetu Mkakati unasifiwa sio tu katika nchi za Afrika bali hata Benki ya Dunia wanatuona kama sisi ndio mfano wa Taasisi ambazo zinatengeneza Mpango Mkakati na zinautekeleza, kuukamilisha,” alisema Mhe. Jaji Mkuu.

Alisema kuwa watekelezaji wakubwa wa Mpango Mkakati ni Watumishi huku akirejea taarifa ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda ambayo imeonyesha ni kwa namna gani ushirikiano wa Watumishi hata katika ngazi za chini walivyoshirikiana kutekekeleza mpango huo na hivyo amewashukuru kwa dhati kwa kupaisha jina la Mahakama.

Aidha; Mhe. Jaji Mkuu alibainisha kuwa moja ya mikakati ya kutekeleza Mpango Mkakati ni pamoja na matumizi ya TEHAMA na kueleza kuwa amedokezwa na Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA kwamba Watumishi wa Mahakama Kanda ya Musoma wanafanya vizuri katika matumizi hayo.

Aliongeza kuwa suala ya uboreshaji wa huduma za Mahakama katika karne ya 21 linapimwa kwa matumizi ya TEHAMA ambapo kwa taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa mashauri yote yaliyopo kwenye Mfumo wa Kusajili Mashauri kwa njia ya Kielektroniki (JSDS II), Kanda ya Musoma yamehuishwa yote kwa asilimia 100 na takwimu hizo ni sahihi.

“Kwa hiyo tunaposema tunaingia kwenye karne ya 21 ya uboreshaji wa huduma za Mahakama, nyinyi ndio mfano hai wa uboreshaji huo, kila kitu kinachofanywa kwenye mtandao kimeenda vizuri, Kanda ya Musoma mmeitikia vizuri sana hivyo lazima tuwasilishe shukrani zetu kwa kuwa mnafanya vizuri sana,” alieleza.

Amewakumbusha Watumishi wa Mahakama kuwa Mpango Mkakati wa pili umeshaanza kufanya kazi hivyo amewaomba kuusoma, kuuelewa na kuutekeleza kwa sababu utasaidia kusukuma mbele azma ya Mahakama ya kuboresha huduma zake kwa wananchi.

“Mwaka 2025 tutasimama na kupimwa tumefanya nini, tumemaliza Mpango Mkakati wa kwanza na sasa hivi Benki ya Dunia wapo wanatupima tumefanya nini. Mahakama itapimwa miaka mitano ijayo na ndio maana tunakimbizana katika kuhakikisha kuwa kila Wilaya inakuwa na jengo la Mahakama ya Wilaya,” alisema.

Jaji Mkuu alibainisha kuwa Mahakama ya Tanzania itahakikisha kuwa maeneo ambayo yamepangwa kufanyiwa ukarabati yanafanyiwa na kwamba Mahakama inaingia katika matumizi ya TEHAMA kama kigezo mojawapo kitakachotumiwa na Benki ya Dunia kwenye upimaji huo.

Hata hivyo; miongoni mwa changamoto zilizoibuliwa na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda ni pamoja na mtandao kuwa chini hali ambayo inasababisha taarifa mbalimbali za mashauri kutopandishwa kwenye mfumo kwa wakati.

Akijibu suala ya changamoto ya mtandao, Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA-Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba alisema kuwa suala hilo limeshaanza kufanyiwa kazi ambapo Mahakama ipo kwenye mchakato wa kuingizwa kwenye mfumo wa TEHAMA unaotumiwa na Serikali.

Katika ziara yake ya siku nne, Mhe. Prof. Juma atatembelea pia maeneo mbalimbali ikiwemo Wilaya ya Serengeti, Tarime na Rorya.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda kama sehemu ya ziara yake ya kikazi aliyoianza leo tarehe 26 Oktoba, 2021.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda wakimsikiliza Jaji Mkuu (hayupo kwenye picha). Kutoka kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Mulokozi Kamuntu,  Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Bw. Festo Chonya na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa huduma za kimahakama, Malalamiko na Maadili-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Annah Magutu.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwasikiliza watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda (hawapo katika picha) alipokuwa akizungumza nao. 


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Musoma, Mhe John Kahyoza (kushoto) akifafanua jambo mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) aliyetembelea jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Bunda leo tarehe 26.10.2021. Pamoja na Jaji Mkuu ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Joshua Nassari (wa tatu kushoto), Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (wa kwanza kulia) na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo ya Wilaya, Mhe. Mulokozi Kamuntu (wa pili kulia).

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Mahakimu Wakazi wa Mahakama katika Wilaya ya Bunda (waliosimama), kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Musoma, Mhe. John Kahyoza na kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda (waliosimama), kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Musoma, Mhe. John Kahyoza na kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma.

Mhe. Jaji Mkuu akipanda mti wa kumbukumbu katika eneo la Mahakama ya Wilaya ya Bunda.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Musoma, Mhe John Kahyoza akipanda mti wa kumbukumbu katika eneo la Mahakama ya Wilaya ya Bunda.

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni