Na Faustine Kapama – Mahakama, Lushoto
Mafunzo ya kuwajengea uwezo na
uelewa Mahakimu Wakazi 200 yanayoendelea katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto (IJA) yameingia siku ya pili leo tarehe 8 Februari, 2022 ambapo Majaji watatu
wa Mahakama Kuu ya Tanzania wamewapitisha washiriki kwenye mada kuu mbili muhimu
zinazohusu utakatishaji fedha na urejeshaji mali zinazopatikana kwa njia ya
uhalifu.
Mmoja wa Majaji hao, Mhe. Awamu
Mbagwa amewaeleza Mahakimu hao kwa kina hatua zinazochukuliwa na mataifa mbalimbali
duniani, ikiwemo Tanzania kupambana na makosa ya uhalifu wa kifedha kwa
kuzingatia athali ambazo hutokea kijamii, kisiasa na kiuchumi. Majaji wengine
walioshirikiana naye katika kuwawezesha washiriki hao ni Mhe. Edwin Kakolaki na
Mhe. Dkt. Zainab Mango.
Akizungumzia kosa la kutakatisha
fedha, Mhe. Mbagwa amesema kuwa utakatishaji fedha ni namna ya kujipatia fedha
haramu, fedha ambazo hutokana na uhalifu na kutafuta njia mbalimbali kuwezesha
fedha hizo zionekane kuwa ni halali.
Kwa mujibu wa Jaji Mbagwa, mtu
anaweza kupata fedha haramu, lakini ili kuzihalalisha anaamua kuziwekeza ama
kwa kununua hisa, kujenga nyumba au kuziingiza kwenye uwekezaji wowote wa
kibiashara au viwanda, lengo likiwa kuonyesha uwekezaji huo ni halali, huku
akijua chanzo cha fedha hizo ni haramu.
Amesema kuwa hapo awali chimbuko la
kosa hilo lilikuwa ni kujihusisha na dawa za kulevya. Hata hivyo, Jaji Mbagwa
amebainisha kuwa mabadiliko kadhaa yalifanyika ili kupanua uwigo wa kupambana
na athali zinazotokana na kosa hilo na kujumuisha makosa yote ya uhalifu wa
kupangwa wa kimataifa, juhudi ambazo zililenga kuwashughulikia wote
wanaonufaika na mazao yanayotokana na makosa tangulizi kwa vile ilikuwa vigumu
kuwapata mapapa wa uhalifu wanaojihusisha na makosa hayo.
“Ili kuendana na matakwa ya sheria
za kimataifa, Tanzania ilitunga sheria ya utakatishaji fedha mwaka 2006. Kwa
mujibu wa sheria hii, utakatishaji fedha ni kosa linalosimama pekee yake bila
mtu kushitakiwa kwanza na makosa mengine tangulizi. Kwa hiyo, siyo lazima
kuthibitisha kosa tangulizi ili kumtia hatiani mtu kwenye kosa la utakatishaji fedha,” amesema.
Sheria hiyo imebainisha makosa
mbalimbali ya utakatishaji wa fedha, ikiwemo mtu yeyote atakaye jihusisha, moja
kwa moja au kwa njia nyingine katika muamala unaohusisha mali itokanayo na mapato
ya fedha haramu akiwa anafahamu au anapaswa kufahamu au alipaswa kufahamu mali
hiyo ni mazao yatokanayo na makosa ya uhalifu ambayo ni msingi wa utakatishaji
wa fedha haramu.
Kwa mujibu wa sheria hii, kosa
jingine ni mtu yeyote atakaye badili, hamisha, safirisha, pitisha mali ikiwa
anafahamu au anapaswa kufahamu au alipaswa kufahamu kuwa mali hiyo ni ya mapato
yatokanayo na uhalifu ambayo ni msingi wa utakatishaji wa fedha haramu, kwa
malengo la kuficha, kupoteza ukweli au chanzo halisi cha mali hiyo kuwa ni
haramu au kumpa msaada mtu yeyote aliye husika katika kufanya kitendo hicho kwa
lengo la kukwepa madhara ya kisheria.
Kosa jingini ni pale mtu yeyote
atakaye ficha, funika ukweli, zuia upatikanaji wa ukweli,
chanzo,mahali,Uhamishaji wa umiliki, mzunguko, au umiliki wa au haki kuhusiana
na mali hiyo, akiwa anafahamu au anapaswa kufahamu au alipaswa kufahamu kuwa
mali hiyo imepatikana kwa mapato yatokanayo na fedha haramu.
Amebainisha pia kuwa ili kuweza
kupambana na makosa hayo ya uhalifu wa kifedha mataifa mbalimbali duniani,
ikiwemo Tanzania, yaliamua kuanzisha sheria ili kukamata mali zote zinazopatikana
kwa njia za kihalifu, malengo yakiwa kuondoa motisha zainazotokana na uhalifu
huo na pia kuzuia wahalifu kufanya uhalifu zaidi.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo (juu na chini) wakitoa michango yao wakati wa kujadili mada zilizowasilishwa.
Washiriki wa mafunzo wakiwa wamegawanyika katika makundi mbalimbali kujadili kwa kina baadhi ya maswali yaliyotokana na uwasilishaji wa mada.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni