Na Emmanuel Oguda-Mahakama, Shinyanga
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe Athuman Matuma jana tarehe 13
Aprili, 2022 ametembelea kikosi kazi maalum cha kumaliza mlundikano
kinachosikiliza mashauri katika Mahakama ya Wilaya Maswa mkoani Simiyu na
kupongeza jitihada zinazoendelea kufanywa.
Mhe. Matuma
ameridhishwa na utendaji kazi wa kikosi hicho pamoja na mikakati iliyowekwa ya
kuhakikisha mashauri ya mlundikano yanamalizika ndani ya siku 14 kama
ilivyopangwa toka yalipooanza kusikilizwa tarehe 11 Aprili, 2022.
Aidha, Jaji Mfawidhi
huyo ameridhishwa na hatua ya wadau wa Mahakama kuendelea kushirikiana na
kikosi kazi hicho ili kumaliza mashauri ya mlundikano katika Wilaya hiyo.
Amesisitiza kuwa
malengo ya Kanda ya Shinyanga ni kumaliza kabisa mashauri ya muda mrefu na
kutoruhusu mlundikano kulingana na mikakati mbalimbali iliyowekwa katika kuzuia
hali hiyo isijitokeze tena.
Kwa upande wao, wananchi wa Wilaya Maswa
wamepongeza jitihada za Mahakama kwa kuamua kuleta Mahakimu toka maeneo mengine
kwa lengo la kuondoa mashauri ya muda mrefu. Wamesema jitihada hizo ziendelee
pia katika maeneo mengine ili wananchi wapate haki zao kwa wakati.
‘’Kesi yangu ina miaka
mitatu hadi sasa, lakini imeanza kusikilizwa na nimeambiwa itamalizika ndani ya
siku 14, ninaipongeza sana Mahakama kwa hatua hii, sasa nina amani kwa vile
shauri langu litamalizika ndani ya muda mfupi,’’ alisema mwananchi mmoja.
Jumla ya Mashauri kumi
ya mlundikano yanaendelea kusikilizwa na yanatarajiwa kukamilika ndani ya siku
14 toka siku ya kuanza kusikilizwa. Itakumbukwa kikosi kazi hiki cha Mahakimu
Wakazi kimemaliza kusikiliza mashauri ya mlundikano katika Mahakama za Hakimu
Mkazi Simiyu na Wilaya Bariadi na kuhamia katika Mahakama ya Wilaya ya Maswa.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athuman Matuma (katikati) akiongea na
Mahakimu wanaounda kikosi kazi maalum cha kumaliza mashauri ya mlundikano
wakati alipotembelea kikosi kazi hicho katika Mahakama ya Wilaya Maswa.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athuman Matuma (aliyenyosha mkono wa kushoto katika picha ya juu na chini) akiongea na
wananchi waliofika kusikiliza mashauri yao Wilaya ya Maswa wakati alipotembelea
kikosi kazi maalum cha kumaliza mashauri ya muda mrefu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Shinyanga Mhe. Athuman Matuma (wa pili
kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na
Mahakimu wanaounda kikosi kazi maalum cha kumaliza mlundikano wa mashauri
wakati alipotembelea kikosi kazi hicho Wilaya ya Maswa. Kutoka kulia ni Hakimu
Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Maswa, Mhe. Christian Lugumira, Hakimu Mkazi
Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Meatu, Mhe. Mohamed Siliti na Hakimu Mkazi Mahakama
ya Wilaya Maswa, Mhe. Enos Misana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni