Na Faustine Kapama– Mahakama
Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Jaji Joseph Sinde Warioba jana tarehe 31 Machi, 2022 alitembelea ujenzi wa
Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma na kushauri Serikali kuanzisha
Mahakama ya Juu (Supreme Court), ambayo ni muhimu kuwepo hapa nchini.
Akizungumza na viongozi wa Mahakama katika eneo la mradi wa
ujenzi huo walioongozwa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma,
Jaji Warioba alionesha kuridhishwa na mpangilio wa jengo hilo ambao unaonesha
uwepo wa sehemu iliyotengwa kwa ajili ya Supreme Court.
“Nimefurahi kuona majengo haya ya Makao Makuu ya Mahakama ya
Tanzania ambayo yanaonesha sehemu kwa ajili ya Supreme Court. Mahakama hii ni
muhimu, ni vema kama tutaianzisha hapa nchini kwetu,” alisema Jaji Warioba. Jengo hilo la Makao
Makuu ya Mahakama ni kubwa na la kisasa kuliko yote ya Mahakama yaliyopo katika
ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kazi za ujenzi katika mradi huo wenye gharama ya billioni
129.7 za Kitanzania unaosimamiwa na Kampuni ya CRJE ya Kichina zilianza Julai
2020 na zinategemewa kumalizika ifikapo tarehe 29 Desemba, 2022.
Kabla ya kutembelea ujenzi huo, Mhe. Warioba ambaye
amehudumu katika nafasi mbalimbali serikalini kabla ya kustaafu alitembelea
Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kuonesha kufurahishwa na mabadiliko
makubwa yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania katika utoaji wa haki kwa
wananchi.
Baada ya kuingia ndani ya jengo hilo, Jaji Warioba hakuweza
kuficha hisia zake baada ya kuona uzuri na uimara wa jengo hilo ambapo alionesha
kuridhika na thamani ya fedha iliyotumika katika ujenzi huo.
Alikuwa na maswali kadhaa ambapo alitaka kujua kama kuna baadhi ya Mahakimu
ambao bado wanatembelea kituo zaidi ya kimoja na kama Mahakama bado ina ajili
Mahakimu wenye Diploma kuhudumu katika Mahakama za Mwanzo.
Katika majibu yake, Mhe. Chuma alimfahamisha Jaji Warioba kuwa
kwa sasa kuna mabadiliko makubwa ambayo yamefanyika katika sekta ya sheria,
ikiwemo Mahakimu wenye Shahada ya Kwanza ya Sheria na Mawakili wa Kujitegemea kuhudumu
katika Mahakama za Mwanzo.
Alibainisha mabadiliko mengine
kama matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), uwepo wa mfumo
wa kusajili mashauri kwa njia ya mtandao (JSDS2), tovuti ya Mahakama
ya Tanzania inayochapisha uamuzi wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, Sheria
na Kanuni (TanzLii) na mfumo wa kielektoniki wa kusajili na kuwatambua Mawakili
nchini(e-wakili).
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (wa pili
kushoto) akimweleza jambo Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba (picha ya juu na chini)
mara baada ya utambulisho.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha (wa kwanza kulia) akimweleza jambo Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba mara baada ya utambulisho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni