Alhamisi, 12 Mei 2022

TEHAMA ILIVYOSAIDIA KUONDOA MASHAURI YA MLUNDIKANO MAHAKAMA YA WILAYA MASWA

 Na Emmanuel Oguda – Mahakama, Shinyanga

Kikosi kazi maalum cha kuondosha mashauri ya mlundikano kikiongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Maswa, Mhe. Christian Rugumira leo tarehe 11 Mei, 2022 kimehitimisha rasmi mashauri yote 11 yaliyokuwa ya mlundikano katika Mahakama hiyo.

Akitoa taarifa ya kumalizika kwa mashauri hayo kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga Mhe. Athumani Matuma, Hakimu huyo amesema mashauri saba kati ya 11 yaliyokuwa yamepangwa kusikilizwa na Mahakimu wanaounda kikosi kazi hicho Kanda ya Shinyanga, yameweza kusikilizwa na kuhitimishwa kwa njia ya ‘’Video conferencing.’’

Amesema jumla ya vielelezo 77 viliwasilishwa kwa njia ya mtandao huku mashahidi wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es salaam, hali iliyopelekea kuokoa fedha ambazo zingetumika iwapo mashahidi hao wangesafiri hadi wilayani Maswa.

“Mashauri yote yaliyopangwa kusikilizwa na kikosi kazi maalum cha kuondoa mlundikano wa mashauri yamesikilizwa na kutolewa uamuzi, hivyo kwa sasa hakuna shauri lolote la mlundikano Mahakama ya Wilaya ya Maswa,” alisema Mhe. Rugumila wakati akiwasilisha taarifa ya kikosi kazi hicho.

Katika taarifa yake, Mhe Rugumira amemshukuru Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga Mhe. Athumani Matuma kwa kuongoza vyema kikosi kazi hicho na kuwa mshauri mkuu wakati kikosi kazi kikiendelea na zoezi la uondoshwaji wa mashauri ya mlundikano katika Kanda hiyo.

Kwa upande wake, Mhe. Matuma amewapongoza Mahakimu hao kwa kazi nzuri ya kukamilisha zoezi la uondoshwaji wa mashauri hayo kwa wakati. Amezitaka Mahakama zingine zenye mashauri ya mlundikano kuwasilisha taarifa haraka iwezekanavyo ili kikosi kazi hicho kiweze kuingia kazini.

Ikumbukwe kuwa Mwezi Februari, 2022 Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, iliunda kikosi kazi maalum kwa lengo la kuondoa mashauri ya muda mrefu ndani ya Kanda hiyo.

Kikosi kazi hicho kilianzia Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu na Mahakama ya Wilaya ya Bariadi na baadae kuhamia katika Mahakama ya Wilaya Maswa ambapo kimehitimisha shughuli hiyo leo.

Aidha, kikosi kazi hicho kitahamia Mahakama nyingine yenye mashauri kama hayo ili kutimiza lengo la Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga kutokuwa na mashauri ya llundikano wa muda mrefu kwa Mahakama zake zote ifikapo mwezi Juni mwaka huu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga Mhe. Athumani Matuma.
Picha ya pamoja ya Mahakimu wakazi walioshiriki katika uondoshwaji wa Mashauri ya mlundikano Mahakama ya Wilaya Maswa wakiongozwa na Mhe. Christian Rugumira (katikati), kutoka kulia ni Mhe Mohamed Siliti, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Meatu, Mhe. Christina Chovenye, Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Kahama, wengine ni Mhe. Catherine Langau, Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Shinyanga na Mhe. Enos Misana, Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Maswa.


Mwonekano wa jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga.

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni