Na Innocent Kansha – Mahakama.
Jaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Dkt. Adam Mambi amewataka
Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani kutumia mafunzo waliyoyapata kuongeza kasi ya
uwajibikaji na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea ikiwa ni pamoja na kupunguza urasimu
usio wa lazima katika kutoa huduma kwa wananchi na watumishi.
Akifunga
mafunzo ya kundi la tatu la washiriki hao yaliyofanyika kwa siku tano tarehe 17
Juni, 2022 katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Dodoma, Mhe. Dkt.
Mambi alisema, Mahakama inategemea kupitia mafunzo hayo yatawaongezea ufanisi
na weledi katika ukusanyaji wa maduhuli, kufanya malipo kupitia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kusimamia matumizi bora ya fedha na rasilimali za Serikali kwa ujumla.
“Tukatumie
mafunzo haya kwa kuwa waadilifu, kuzingatia sheria, kanuni na taratibu
zinazoongoza utumishi wetu na pengine mkawe watoa elimu hii kwa watumishi
wengine kila fursa ya kufanya hivyo inapopatikana”, alisisitiza Jaji Mambi
Hivyo
kwenu, ni wajibu na dhamana mliyokabidhiwa kufanya kazi mlizojifunza kwa
nidhamu ili kutatua changamoto zilizopo na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa
majukumu na kutumia mfumo wa TEHAMA katika kazi, kuzingatia uadilifu, kulinda usalama wa fedha
na matumizi sahihi ya mitandao.
“Washiriki
wa mafunzo mkiwa kama wasaidizi wa Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
katika kusimamia matumizi bora ya fedha, naamini mafunzo haya yatawasaidia sana
katika kutekeleza majukumu yenu na kurahisisha kazi ya Ofisi ya CAG”, Jaji
Mambi aliongeza.
Dkt.
Mambi akawakumbusha washiriki hao mambo ya msingi ya kuyazingatia ambayo ni
uadilifu, weledi na kuongeza bidii katika kazi ikiwa ni pamoja na kutumia vipawa
vyao kubuni njia sahihi za kutatua changamoto. Ushirikianao kama timu na
nidhamu ya dhati katika utekelezaji wa majukumu wakiongozwa na uzalendo na
uchamungu.
Jaji
Mambi alisema, mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa sheria ya miamala ya
kielektroniki ya mwaka 2015 pamoja na sheria ya Serikali mtandaoya 2019. Sheria
zote mbili zinaruhusu malipo kufanyika kupitia mtandao (e-payment) na usimamizi
wa fedha kupitia mtandao (e-auditing)
Sheria
hizi zinatoa mamlaka ya kufanya malipo na kusimamia fedha kwa kutumia mfumo wa
TEHAMA. Mathalani vifungu vya 13, 14, na 15 vya sheria inayosimamia miamala ya
kielektroniki ya mwaka 2015, vinaruhusu malipo ya fedha kufanyika kwa njia ya
mtandao kama sehemu ya utekelezaji wa Serikali mtandao. Vilevile vifungu vya 31, 35, na 64 vinatambua
na kuruhusu malipo na usimamizi wa fedha kufanyika kwa njia ya kielektroniki au
mtandao, aliongeza Jaji Mambi.
Aidha,
Dkt. Mambi alisema mafunzo hayo yalijikita katika kuongeza uzoefu wa namna bora
ya kutumia TEHAMA katika masuala mazima ya fedha kama vile kufanya malipo,
kupokea au kukusanya fedha kwa njia ya mtandao na kufanya ukaguzi kwa kwa njia
hiyo.
Kwa
upande wa Mpango Mkakati wa Mahakama awamu ya pili, Jaji Mambi aliwakumbusha
washiriki kuwa mafunzo hayo yameutafsiri mpango huo kwa vitendo katika
kuhakikisha usimamizi na utoaji wa huduma ya haki inayomlenga mwananchi anayehudumiwa
inaendelea kwa kasi na yenye kufuata misingi ya uadilifu, uwajibikaji, weledi bila
kusahau uzalendo.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia hotuba ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Dkt. Adam Mambi (hayupo pichani) wakati wa ufungaji mafunzo hayo.
(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni