Na Brian Haule-Mahakama, Songea
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Yose Mlyambina jana
tarehe 10 Juni, 2022 amezindua anuani ya makazi katika Jengo la Mahakama Kuu
Songea na kuwahimiza Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama zote za Hakimu Mkazi na
Wilaya kutekeleza agizo la Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Khamis
Juma la kuwekaji vibao vya anuani hizo katika Mahakama zao.
Akiongea
katika hafla ya uzinduzi huo, Jaji Mfawidhi alisema, “Ni rai yangu kuwa
tutashiriki kikamilifu kwenye utekelezaji wa anuani za makazi kwa maendeleo
yetu na jamii kwa ujumla. Tukumbuke pia hili ni agizo la Jaji Mkuu wa Tanzania
alilolitoa katika ziara yake ya Mahakama, Kanda ya Tanga. Hivyo nami naagiza
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea na Mahakimu Wakazi
Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya Songea, Tunduru, Namtumbo, Mbinga na Nyasa
kutekeleza hili kwa haraka na kuhakikisha Headed letters (vichwa vya barua)
zetu ziwe na anuani za makazi,” alisema.
Aidha
Mhe. Mlyambina aliwaeleza watumishi wa Mahakama waliohudhuria hafla hiyo kuwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko katika utekelezaji wa mchakato wa anuani za
makazi nchi nzima, hivyo kutokana na umuhimu wa zoezi hilo Mahakama ya Tanzania
nayo ni sehemu ya taasisi ambazo zinapaswa kuwa na anuani ya makazi kwa sababu
ya faida mbalimbali.
Alizitaja
faida hizo kama utambulisho wa maeneo kwa urahisi, kufikiwa kwa maeneo mengi,
ikiwemo Mahakama kwa ajili ya huduma mbalimbali kwa wadau, upangaji na
usimamizi wa mipango ya kutoa huduma kwa wananchi, utoaji wa huduma za dharura
kwa wananchi na kukabiliana na maafa mbalimbali, kurahisisha mawasiliano baina
ya taasisi, wadau na wananchi kwa ujumla, kuimarisha ulinzi na usalama na
vyombo vya dola kufuatilia endapo kuna changamoto yoyote, kufahamu athari
inayoweza kujitokeza endapo ataingia mgeni, kuepusha migogoro ya mipaka na
majirani na upatikanaji wa hati za viwanja.
“Tukiwa
tunaelekea kwenye Mahakama Mtandao, anuani za makazi zitarahisisha malengo yetu
kufikiwa kwa wakati kwani kutakuwa na urahisi wa kufikiwa, lakini pia anuani za
makazi zinakwenda sambamba na upangaji na usimamizi wa mipango ya maendeleo na
utoaji huduma, zikiwemo za mawasiliano kama vile usambazaji wa Mkonga wa
Taifa,” alisema Jaji Mfawidhi huyo.
Mhe.
Mlyambina alitumia fursa hiyo kuwaasa watumishi wa Mahakama ya Tanzania Kanda
ya Songea kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Uviko-19. “Niwaombe
watumishi wenzangu tuendelee kujitahadhari na ugonjwa wa Uviko-19 kwani kinga
ni bora kuliko tiba,” alisema.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Yose Mlyambina (kushoto)
akiwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Upendo Madeha (kulia) wakati wa uzinduzi wa
kibao cha anuani ya makazi katika jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Songea.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Yose Mlyambina (picha ya juu na mbili chini) akiongea na watumishi wa Mahakama Kanda ya Songea wakati wa uzinduzi wa anuani ya makazi katika jengo la Mahakama Kuu Songea.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni