Jumatatu, 13 Juni 2022

MCHAKATO KUELEKEA MAHAKAMA MTANDAO WASHIKA KASI; KALIUA NAYO YAPOKEA VIFAA VYA TEHAMA

Na Amani Mtinangi – Mahakama Kuu Tabora

Katika jitihada za kuendeleza azma ya Mahakama ya Tanzania ya kuwa Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’, Mahakama ya Wilaya Kaliua imepokea vifaa mbalimbali vya TEHAMA ikiwemo kompyuta za mezani, luninga, ‘printer’, mashine ya kurudufisha na kompyuta mpakato ili kurahisisha kazi ya utoaji haki nchini kwenda kidijitali.

Vifaa hivyo vilivyowasilishwa mwishoni mwa wiki iliyopita na kampuni ya ‘COMSKILLS Company Ltd’ kwa niaba ya uongozi wa Mahakama vitatumiwa katika jengo jipya la Mahakama hiyo linalotarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu.

Makabidhiano hayo ya vifaa hivyo yalishuhudiwa na Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu- Kanda ya Tabora, Bw. Ginaweda Nashon kwa niaba ya uongozi wa Kanda hiyo pamoja na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kaliua, Mhe. Anna Chilongola kwa niaba ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya hiyo.

 Vifaa hivyo vilivyopokelewa sio tu vitakuwa mwarobaini wa changamoto ya uhaba wa vifaa katika Mahakama hiyo, bali pia vitaongeza ufanisi na kasi ya usikilizaji wa mashauri katika wilaya huyo.

 Wakati huo huo, Kaimu Mtendaji wa Kanda hiyo, Bw. Nashon alifanya pia ukaguzi wa Mradi wa ujenzi wa jengo la Mahakama Wilaya Kaliua. Ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 68 ambapo kwa sasa hatua iliyofikiwa ni ya upauaji na kufunga dari kupaka rangi baadhi ya maeneo.

Mradi huo unaotarajia kukamilika mwanzoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, ni matokeo ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021-2024/2025 ambao pamoja na mambo mengine, umelenga kuboresha miundombinu yake ili kuweka mazingira rahisi na wezeshi ya utoaji haki kwa watu wote na kwa wakati.

Katika ukaguzi huo, Bw. Nashon amesisitiza umuhimu wa kazi hiyo kumalizika kwa wakati na kumuelekeza Mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi ili kumaliza mradi huo kwa wakati na hatimaye jengo hilo liweze kutumika kwa malengo kusudiwa.

Mahakama hiyo iliyoanza kufanya kazi Oktoba, 2020 haina majengo yake yenyewe ambapo tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikitumia majengo yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kaliua.

 Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Tabora, Bw. Ginaweda Nashoni (mwenye miwani) pamoja na Mhe. Anna  Chilongola na Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Bi. Emiliana Surumbu (aliyesimama katikati) wakihakiki vifaa mbalimbali vilivyowasilishwa kwa ajili Mahakama ya Wilaya Kaliua.

Uhakiki wa vifaa ukiendelea kabla ya kuvipokea rasmi.

Muonekamo wa jengo la Mahakama ya Wilaya Kaliua ambalo lilikaguliwa na Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Tabora, Bw. Ginaweda Nashon. Ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 68, kwa sasa hatua iliyofikiwa ni ya upauaji na kufunga dari kupaka rangi baadhi ya maeneo. 

 Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Tabora, Bw. Ginaweda Nashon akipokea maelezo kutoka kwa Msimamizi wa Mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kaliua.

Muonekamo wa jengo la Mahakama ya Wilaya Kaliua kwa nyuma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni