Jumatatu, 27 Juni 2022

MAHAKIMU MKOANI KAGERA WAASWA KUZINGATIA MAADILI

 Na Ahmed Mbilinyi – Mahakama, Bukoba

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga amewaasa Mahakimu wa Mahakama Mkoa wa Kagera kuelewa na kuzingatia kanuni za maafisa wa Mahakama kwa kuwa ni miongoni mwa miongozo muhimu katika kutekeleza majukumu yao.

Mhe. Kilekamajenga ametoa wito huo katika ufunguzi wa mafuzo ya ndani ya siku moja yaliyoandaliwa na Mahakama Kuu, Kanda ya Bukoba, kuwaleta pamoja Mahakimu wote wa Mahakama Mkoa wa Kagera. Mafunzo hayo yalifanyika mkoani hapa tarehe 25 June, 2022 kwa lengo la kushirikishana, kubadilishana ujuzi, kukumbushana majukumu na viwango bora vya utendaji kazi.

Mafuzo hayo yalihusisha mada mbalimbali zikiwamo Maadili (Ethics) kwa Maafisa wa Mahakama, mada ambayo iliwasilishwa na Mhe. Kilekamajenga na mada inayohusu Uandishi Bora wa Nakala za Hukumu iliyowasilishwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Kanda hiyo, Mhe Angaza Mwipopo.

Mada nyingine ilihusu Naona Bora ya Kushughulikia Kesi za Mirathi iliyowasilishwa Jaji mwingine kutoka Kanda hiyo, Mhe. Emmanuel Ngigwana,  mada iliyohusu makosa ya mara kwa mara yanayojitokeza kwenye uendeshwaji wa kesi za jinai iliyotolewa na Jaji kutoka Kanda hiyo, Mhe Ayub Mwenda, huku mada kuhusu Utekelezwaji wa Hukumu (Execution) ambayo iliwasilishwa Msaidizi wa Jaji, Mhe Edwin Kamaleki.

Sambamba na hilo, kulikuwa na mada nyingine zilizotolewa na maafisa waalikwa kutoka Ofisi za Takukuru (PCCB) na Ofisi ya Waangalizi wa Adhabu Mbadala.

 Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga akiwasilisha mada kuhusu Maadili (Ethics) kwa maafisa wa Mahakama.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,  Kanda ya Bukoba, Mhe. Angaza Mwipopo akiwasilisha mada kuhusu Uandishi bora wa Nakala za Hukumu.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Emmanuel Ngigwana akiwasilisha mada kuhusu Namna Bora ya Kushughulikia Kesi za Mirathi.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Ayub Mwenda akiwasilisha mada ya makosa ya mara kwa mara yanayojitokeza kwenye uendeshwaji wa kesi za jinai.
Sehemu ya Mahakimu wa Mkoa wa Kagera (juu na chini) wakimsikiza kwa makini mtoa mada ya Maadili (Ethics) kwa Maafisa wa Mahakama, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga (hayupo kwenye picha).










 






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni