Na Innocent Kansha – Mahakama, Dododma
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Gerson Mdemu
amewasisitiza Wahasibu na Wakaguzi wa ndani kutumia taaluma, maadili, miongozo,
sera na sheria kurahisisha utelelezaji wa dira ya Mahakama inayohusu
Upatikanaji wa Haki kwa Wakati na kwa Wote.
Akifunga mafunzo ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani yalifanyika kwa siku tano katika
Ukumbu wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Jijini Dodoma jana tarehe 3 Juni 2022
Jaji Mdemu alisema, dira hiyo haiwezi kutekelezeka iwapo mifumo ya kihasibu
waliyojifunza haitaondoa usumbufu kwa wadaawa kufanya malipo mbalimbali ya
usajili wa mashauri na nyaraka za kimahakama kwa ufanisi, kulipa mirathi kwa
wakati na watumishi wa ndani kulipwa stahiki zao bila usumbufu na kucheleweshwa.
“Pengine
jambo la msingi ambalo mnatakiwa kulifahamu na kupitia mafunzo haya mmelifahamu
ni kuwa upatikanaji wa haki kwa wakati na kwa wote haliwahusu maafisa wa Mahakama tu, bali hata ninyi mnahusika kwa asilimia mia moja katika utoaji
wa huduma ya haki unaomlenga mwananchi na hivyo tukakatimize kwa vitendo”,
aliongeza Jaji Mdemu.
Mhe. Mdemu akatoa rai kwa Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani kutumia ujuzi walioupata katika mafunzo hayo kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutatua changamoto za utoaji wa huduma za kihasibu ili kurahisisha na kuondoa usumbufu kwa wadaawa wanaowapa huduma, kwani TEHAMA ndiyo msingi wa kurahisisha upatikanaji wa huduma, kwa kuwa ninyi ndo mmefunzwa kuhusu matumizi ya hiyo mifumo basi msiende kuwa msiwe kikwazo cha utoaji huduma bora kwa wadaawa.
"Mahakama ya Tanzania inanuwia kuwa na maamuzi bora ya kimahakama ambapo imejiwekea malengo ya kukuza uelewa wa misingi ya taaluma ya kisheria na kuongeza ujuzi kwa watumishi wa mahakama. Katika kutekeleza malengo hayo, Mahakama imejiwekea mkakati wa kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama wa ngazi zote. Mmejengewa uwezo kwenye eneo lenu la kihasibu. Sasa hakutakuwa na kisingizio cha kuchelewesha huduma, hususani masuala ya mirathi ambayo yanahitimisha maamuzi yanayotolewa na Mahakimu na Majaji"', aliongeza Jaji Mfawidhi
Kuhusu
mada zilizofundishwa Jaji Mdemu alisema maeneo yote yaliyofundishwa na
wawezeshaji ni muhimu sana na yanahusu utekelezaji
wa majukumu yao kama Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani kitaaluma na kimaadili. "Mmepewa
nyenzo muhimu za utekelezaji kwenye maeneo mengine yaliyo nje ya taaluma yenu lakini
hayaepukiki katika kuhakikisha mnatimiza wajibu wenu katika kutoa huduma ya
kihasibu. Mlikuwa na majadiliano mbalimbali ambayo yaliwawezesha kubadilishana
uzoefu katika kazi zenu, mkayatumie yote mliyoyapata katika kufanyia kazi", alisema Jaji Mdemu.
Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021-2024/2025 ambapo katika Tunu ya Tano kuhusu weledi, Mahakama itatekeleza majukumu ya utoaji haki kwa umahiri na ufanisi. Aidha, ndani ya Mpango Mkakati huo, katika nguzo ya kwanza inayohusu utawala, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali, moja ya lengo ni kuwajengea uwezo watumishi wa ngazi zote.
Sehemu ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani wakifuatilia mada ya Mpango Mkakati wa Mahakama awamu ya pili wakati wa mafunzo hayo yalifanyika kwa siku tano katika Ukumbu wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Jijini Dodoma.
Sehemu ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani wakifuatilia mafunzo hayo.
(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni