Na Lusako Mwang’onda-Mahakama, Iringa
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Dkt. John Utamwa amewahimiza watumishi kuyatunza majengo yanayojengwa hapa nchini ili kuunga mkono juhudi za Mahakama na Serikali ya Tanzania kwa ujumla katika kuboresha miundombinu hiyo.
Mhe. Dkt. Utamwa alitoa wito huo hivi karibuni wakati
wa uzinduzi wa jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo Lugarawa lililopo katika Wilaya
ya Ludewa mkoani Njombe.
Jaji Mfawidhi huyo alibainisha kuwa Serikali inatumia
pesa nyingi katika kujenga majengo mbalimbali ya Mahakama, hivyo ni wajibu wa
kila mtu na hasa watumiaji ambao kwa kiasi kikubwa ni watumishi wa Mahakama
kuhakikisha kuwa yanatunzwa vyema.
“Litakuwa ni
jambo la aibu kuona hili jengo ambalo tunalizindua likiwa safi hivi, halafu
baada ya muda tunarudi hapa na kulikuta limechafuliwa kwa namna yoyote. Ni wajibu
wetu watumiaji wa majengo haya kuhakikisha kuwa yanabaki kuwa safi na salama,”
alisema.
Sherehe za uzinduzi wa Mahakama hiyo zilihudhuliwa na
viongozi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Serikali na wananchi.
Baadhi ya viongozi wa Mahakama waliohudhuria sherehe
hizo ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe.
Maximillian Malewo, Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi
Chamshama, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa,
Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Yusuph Msawanga na Hakimu Mfawidhi
wa Mahakama ya Wilaya ya Ludewa, Mhe. Isack Ayengo.
Sherehe hizo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali
wa vyombo vya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ludewa, wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya
hiyo Mhe. Andrea Tsere.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni