Alhamisi, 28 Julai 2022

MAHAKAMA KUU KANDA YA MWANZA YAJADILI NA WADAU MIKAKATI YA KUSUKUMA MASHAURI

 Na Stephen Kapiga –Mahakama, Mwanza

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza leo tarehe 28 Julai, 2022 imefanya kikao cha kusukuma mashauri kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kujadili mikakati ya pamoja ili kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi.

Kikao hicho kilichoongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama kutoka Kanda hiyo, Mhe. John Kahyoza kilianza kwa kupokea taarifa ya utendaji kutoka kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Chiganga Mashauri ambaye alionyesha kuwa kasi ya ufunguaji wa mashauri kwa upande wa Mahakama Kuu imepanda kwa wastani wa mashauri 60 kwa kila mwezi.

“Kasi hii inaendana na usikilizaji na umalizaji wa mashauri kwa wakati. Nawapongeza Majaji kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na ile ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa kwa ushirikiano mzuri katika kasi ya usikilizaji wa mashauri, hivyo kuwezesha kiwango cha mashauri ya mlundikano kushuka kwa asilimia 5 mpaka sasa ukilinganisha na mwezi Machi tulivokutana hapa,” alisema.

Kuhusu uendeshaji wa mashauri kwa njia ya TEHAMA, Naibu Msajili huyo alibainisha kuwa kwa kipindi cha Machi hadi Julai 2022, jumla ya mashauri 44 ya jinai yameendeshwa kwa njia ya mfumo wa video conference na hivyo kuokoa muda kwa wadaawa na pia gharama za uendeshaji kwa Mahakama.

Akizungumza katika Kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa na Majaji wote wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Mahakimu Wafawidhi wote wa Mahakama za Mkoa na Wilaya kutoka Mwanza na Geita, Polisi, Magereza, Ustawi wa Jamii, Mawakili wa Serikali na kutoka Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Jaji Mfawidhi huyo aliwasihi Magereza kuenda na kasi ya Mahakama katika matumizi ya TEHAMA kwa vile teknolojia hiyo kwa sasa haikwepeki.

“Ndugu zangu wa Magereza, kwa sasa matumizi ya TEHAMA kwa upande wa Mahakama hayakwepeki. Nawaomba na kuwasisistiza sana mtumie TEHAMA haswa katika ufunguaji wa rufaa za wafungwa, kwani hii itasaidia kuepuka kuchelewesha rufaa hizo na pia hata usahihi wa taarifa na utunzaji wake ni wa uhakika kwa vile kila taarifa inakuwa imehifadhiwa katika mfumo,” alisema.

Aidha, Mwenyekiti wa Kikao aliwataka Mkoa wa Geita kuweka mkakati bora baina ya polisi na waendesha mashtaka ili kusukuma kwa haraka mashauri ya mauaji ambayo kwa kiwango kikubwa yapo katika Mkoa huo, hivyo kupelekea mlundikano. Kadhalika aliwataka Mahakimu katika Mahakama za chini kuwa na mfumo bora wa kuondokana na mashauri ya mlundikano.

“Siyo Geita tu nawaambia haya hata nyie ambao kwa sasa hamna mashauri ya aina hii, ni vizuri mkawa na namna bora ya kufanya uchambuzi na kuzuia mlundikano kwa kuyatambua mapema mashauri ambayo huenda yataingia katika hatua hiyo. Pia ni vizuri kwa hayo machache yalipo kuyaendesha kwa njia ya vikao ili kusafisha kabisa mlundikano mlionao,” alisema.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Mwanza ambaye aliwaomba wale wote wenye mlundikano kuwasiliana na ofisi yake ili waweze kuwashirikisha waendesha mashtaka kupanga namna bora ya kushirikiana katika kuondoa mashauri hayo mahakamani, huku waendesha mashtaka hao wakiomba uwepo wa ratiba nzuri ya Mahakimu kwani wao wapo tayari kushirikiana na Mahakama katika mkakati huo.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii, Bw. Magnus Rwekaza ameipongeza Mahakama kwa kuzingatia matumizi ya adhabu mbadala kwani kwa sasa inasaidia kupunguza msongamano katika Magereza, hivyo akawasihi Mahakimu ambao bado hawajaanza kutumia utaratibu huo kufanya hivyo kwa vile utasaidia wote wakiwa kama wadau wa haki jinai.

Akizungumzia upande wa Mawakili, Mwenyekiti huyo aliwasisitiza kuanza kutumia fomu maalumu ya maelezo ya shaidi kwani itasaidia katika usikilizaji kwa haraka zaidi na kuondoa zile mbwembwe za kuhoji mashahidi ambao zimekuwa zikichukua muda mrefu wa Mahakama. Amesema matumizi ya fomu hiyo pia itasaidia kuchuja mashahidi na kubaki na wale ambao ni muhimu katika mashauri yatakayokuwa yanaletwa mahakamani, hivyo kuchochea kumalizika kwa haraka.

Aidha, Mhe. Kahyoza aliwasihi wale wote wanaoleta mashauri ya mirathi kuwasilisha cheti halisi cha kifo wakati wa ufunguaji, huku akionya shauri hilo halitafunguliwa bila kuwepo wa nyaraka hiyo muhimu au wosia halisi. Amesema hatua hiyo itaepusha wale wenye tabia ya kufungua mirathi zaidi ya Mahakama moja pale wanapoona wanaelekea kushindwa katika Mahakama zingine na pia kuondoa mgongano wa uwepo wa mashauri mengi ya marehemu mmoja.

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. John Kahyoza akiwa katika kikao cha wadau wa Mahakama cha kusukuma mashauri kilichofanyika leo tarehe 28 Julai, 2022.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Mwanza, Bw. Steven Kitale (kushoto) akizungumza jambo na Wakili Amri Linus baada ya kikao cha wadau wa Mahakama cha kusukuma mashauri.

Sehemu ya wajumbe waliohudhuria na kushiriki kikao cha kusukuma mashauri Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza (juu na chini) wakifuatilia mawasilisho na michango mbalimbali iliyotolewa wakati wa kikao.

 

Sehemu ya wajumbe wakiwa katika majadiliano mbalimbali nje ya ukumbi baada ya kumaliza kikao cha kusukuma mshauri Mahakama Kuu Mwanza.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni