Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Mahakama ya Tanzania, Mkoa wa Morogoro leo tarehe 27
Julai, 2022 imeendelea na mpango wake wa kutoa elimu kwa wananchi katika
masuala mbalimbali ya kisheria, ikiwemo kusikiliza mashauri kwa njia ya
mtandao.
Akitoa elimu hiyo kwa wananchi waliofika katika
Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoani hapa, Afisa Tekinolojia Habari na
Mawasiliano (TEHAMA), Bw. Tamimu Husein alisema njia ya usikizaji wa mashauri
kwa mtandao ni rahisi ambayo mtu huweza kuitumia akiwa sehemu yeyote na akapata
huduma ya kimahakama.
Akijibu swali la Mwananchi William Makunganya
aliyetaka kujua namna ambavyo Mahakama imejipanga endapo mshatakiwa akitiwa hatiani
baada ya hukumu yake kusomwa kwa njia hiyo akiwa nje kwa dhamana, Msaidizi wa
Sheria wa Jaji, Mhe. Lameck Mwamkoa alisema kazi ya Mahakam ni kutafsiri sheria.
“Vyombo husika vitafanya kazi yake ya kumkamata
mshtakiwa na kumpeleka sehemu husika ili akapatiwe haki yake endapo kama
itakapotokea changamoto kama hiyo,” alisema.
Hatua hiyo ya elimu iliyotolewa na Mahakama imepokelewa
vizuri na wateja ambao wengi wameonesha shauku ya kutaka kujua zaidi ili iwe
rahisi kwao kufuatilia mashauri yao wakiwa katika maeneo tofauti tofauti.
Mkazi mmoja aliyejulikana kama Sudi Mindu alitoa
pongezi zake kwa Mahakama na kusema kuwa sasa wamerahisishiwa huduma na
kupunguziwa gharama za kusafiri ili kufuata huduma mahakamani.
Usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya mtandao sasa
unapatikana kwa wateja wote wenye simu janja na hata wasio kuwa nazo wanaweza
kufika katika Mahakama iliyo karibu nao li waweze kuunganishwa na kusikiliza
kesi wakuwa huko huko waliko. Hii ni hatua nyingine kubwa ambayo Mahakama
imepiga ili kuendana na mapinduzi makubwa yaliyoko katika tekinolojia.
Afisa Tekinolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bw.
Tamimu Husein akitoa elimu kwa wananchi namna wanavyoweza kusikiliza mashauri kwa
njia ya mtandao bila kufika mahakamani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni