Na Festo Sanga-Mahakama, Kigoma
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha amewasihi
wadau wa haki jinai kutotumia adhabu mbadala katika mazingira ambayo jamii
itawashangaa kwa vile matumizi ya adhabu ya aina hiyo sio matakwa ya mtu
binafsi wala taasisi fulani bali ni matakwa ya kisheria.
Mhe.
Mlacha alitoa wito huo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili yaliyoanza tarehe
29 Julai 2022 yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani- Idara ya Huduma za Uangalizi
Mkoa wa Kigoma yakiwashirikisha wadau wa haki jinai kutoka Mahakama, Ofisi ya
Taifa ya Mashtaka, Huduma za Uangalizi, Polisi, Magereza na Ustawi wa Jamii.
“Adhabu
mbadala haitakiwi kutolewa kiholela kwani inaweza kuharibu jamii. Adhabu
ya miaka chini ya mitatu sio kigezo
pekee, zingatieni aina ya kosa lililotendeka, jamii ina mtazamo gani na tabia
za mhusika,” Jaji Mfawidhi huyo alisisitiza.
Aliongeza
kuwa Utekelezaji wa adhabu mbadala utawaepusha wahalifu wa makosa madogo kuiga
tabia mbaya ya wahalifu sugu waliopo gerezani na pia utapungunguza msongamano
na gharama za kutunza wafungwa gerezani.
Aidha,
Mhe. Mlacha alibainisha kuwa utaratibu huo utatoa fursa kwa wahalifu wa makosa
madogo kuwa karibu na familia zao na kutekeleza wajibu wao wa kifamilia na
kijamii na utaiwezesha jamii kushiriki katika urekebishaji wa wahalifu na
kunufaika moja kwa moja na shughuli wanazozifanya na pia kuwezesha utengamanisho
wa wafungwa na jamii (re-integration of offenders into the community).
Naye
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Huduma za Uangalizi, Bw. Charles Nsanze alisema kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kutoa msukumo mpya wa
utekelezaji na usimamizi wa adhabu mbadala katika Mkoa wa Kigoma kwa kusaidia
kujenga uelewa wa pamoja juu ya utekelezaji wake na taratibu za kisheria katika
utoaji wa adhabu hiyo ambayo ni moja ya mikakati ya kujenga ushirikiano
miongoni mwa wadau wa Haki Jinai kutekeleza majukumu yao ya kila siku ya kuwahudumia
wananchi.
Mafunzo
hayo yanalenga kutekeleza maelekezo ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma ambayo amekuwa akiyatoa
kwa nyakati tofauti akihimiza
matumizi ya adhabu mbadala kwa wahalifu wasio hatarishi kwa usalama wa raia na
mali zao, huku akiwataka wadau kutekeleza adhabu hiyo kwa wahalifu wote
waliotimiza vigezo vya kisheria.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha akiongea na waandishi wa Habari mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili yanayohusu adhabu mbadala kwa wadau wa Haki jinai mkoa wa Kigoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni