Jumatano, 13 Julai 2022

TUMIENI USULUHISHI KUPUNGUZA MIGOGORO; JAJI MKUU

Na Magreth Kinabo – Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amekishauri Kituo cha usuluhishi cha Mahakama Kuu ya Tanzania, kulipatia uzito suala la usuluhishi kwa kuwa linapunguza migogoro mahakamani ili kusaidia nchi kuwa na amani, utulivu na kukuza uchumi.

Akizungumza leo tarehe 13 Julai, 2022 kwenye ofisi ya kituo hicho, iliyopo kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi, Jijini Dar es Salaam, alipofanya ziara ya kukitembelea, amesema bado suala la usuluhishi lina nafasi ya kuchukuliwa uzito unaostahili.

“Suala la usuluhishi ni muhimu likapewa nafasi kwa ngazi zote za Mahakama kwa kuwa linaleta matokeo chanya baina ya pande zote mbili za mgogoro,” alisema Prof. Juma na kuongeza kwa kuwataka viongozi alioambatana nao kutoka Makao Makuu ya Mahakama kuanza kulifanyia kazi suala hilo mara moja.

Akizungumzia kuhusu suala la safari ya Mahakama kuelekea Mahakama Mtandao, alikishauri kituo hicho kuongeza jitihada za kutumia mifumo ya kidijitali kama ilivyo katika nchi ya Bahamas, ambayo sasa kila kitu kinaenda kidijitali.

Jaji Mkuu pia alikishauri kituo hicho kuangalia sheria mbalimbali ambazo zimetungwa ili kuwezesha mifumo kuweza kuokoa muda wa kusikiliza mashauri, hivyo mashauri yanaweza kusikilizwa kwa wakati mwingine nje ya Mahakama. Pia alikitaka Kituo hicho kufanya utafiti wa muda unaopotea ili kuweza kupunguza muda wa usuluhishi na kuja na mapendekezo.

Alitaka watumishi wa kituo hicho kupatiwa mafunzo ili kuweza kuongeza uelewa zaidi juu ya suala hilo, ambapo Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Mustapher Siyani aliahidi kulifanyia kazi.

Kwa upande wake Kaimu Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma amesema kuwa, matumizi ya njia hiyo ya kusuluhisha migogoro inaongeza wigo wa upatikanaji wa haki kwa wakati kwa gharama nafuu, ustaarabu na amani bila kufungwa na sheria au taratibu za kiufundi.

Alitolea mfano katika nchi ya Singapore kuwa asilimia 90 ya mashauri yanaweza kumalizika kwa njia ya usuluhishi na asilimia 10 ya mashauri nchini humo, ndiyo humalizika kwa shauri kusikilizwa hadi kufikia hatua ya hukumu na Marekani hutumia njia ya usuluhishi kwa asilimia 60.

“Uanzishaji wa kituo hiki ni mwendelezo wa utekelezaji na upimaji wa matumizi ya njia  hii mbadala kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuweza  kueneza utekelezaji wenye tija katika ngazi zote za Mahakama," amesema Jaji Maruma.

Aliongeza kwamba, kuanzia mwaka 2015 hadi kufikia Juni mwaka huu, Kituo kimesuluhisha mashauri yapatayo 1,670, ambapo kati ya hayo mashauri 285 yaliweza kusuluhishwa na kumalizika kwa njia hiyo.

Mhe. Maruma alisema katika kipindi cha miaka saba tangu kituo hicho kianzishwe mwaka 2015 kimekuwa kikitekeleza hatua hiyo ya usuluhishi wa mashauri kutoka Masjala za Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Divisheni ya Ardhi ikiwa ni eneo la majaribio kuweza kusaidia kutatua migogoro mingi iliyolundikana katika masjala hiyo.

Alisema toka kuanzishwa kwake mwaka 2015 hadi Juni 30, mwaka huu, kituo hicho kimepokea jumla ya mashauri 1,742 na kusuluhisha mashauri 1,670 na kubaki na mashauri 71 mpaka Juni 30, mwaka huu. Kati ya mashauri 1,670 yaliyosuluhishwa ni mashauri 285 sawa na asilimia 17. Asimilia 15 usuluhishi wake ulifanikiwa kwa kiasi na twakimu zinaendelea kuonyesha kwamba mashauri 1,265 sawa na asilimia 82 usuluhishi wake ulishindikana.

Akizungumzia kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) alisema  kituo hicho  kimeweza kuratibu usuluhishi kupitia Mkutano Mtandao, hivyo kutoka mwaka 2020 mpaka Juni 2022 mashauri 33 yamesuluhishwa kwa njia hiyo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa kituo hicho. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani na (kulia) ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama Kuu, Zahra Maruma.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama Kuu, Mhe. Zahra Maruma (wa kwanza kushoto) akitoa taarifa ya utendaji kazi ya kituo hicho.

 

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akipokelewa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani kwa ajili ya kuanza ziara katika Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama Kuu leo Jijini Dar es Salaam.

Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Kevin Mhina akizungumza jambo kwenye mkutano huo.

Baadhi ya watumishi wa kituo hicho wakimsikiliza (Jaji Mkuu hayupo pichani).

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Mahakama ya Tanzania. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani na (kulia) Kaimu Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama Kuu, Mhe. Zahra Maruma. 

(Picha na Mary Gwera - Mahakama)

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni