Na Ahmed Mbilinyi – Mahakama, Bukoba
Rais wa Chama
cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Mwanza, Mhe John Kahyoza amesisitiza
kuimarishwa kwa matawi ya chama hicho kote nchini.
Mhe. Kahyoza alitoa wito huo hivi karibuni
katika mkutano wa JMAT Tawi la Kagera ambapo alikuwa mgeni rasmi. Akizungumza katika
mkutano huo, Mwenyekiti huyo alisisitiza matawi ya JMAT kuwa na utaratibu wa
kutembeleana na kubadilishana uzoefu ili kuongeza tija katika utendaji kazi. Kadhalika,
aliwakumbusha wanachama umuhimu wa kutoa michango yao ya kila mwezi.
Awali, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga, ambaye ni mlezi wa
JMAT Tawi la Kagera, aliwaeleza wajumbe kuwa uwepo wa chama hicho ni muhimu kwa
kuwa hakuna sehemu nyingine ya wao kujisemea. Alimshukuru Mhe. Kahyoza kwa kukubali
kuwa mgeni rasmi katika mkutano huo pamoja na kuwa na majukumu mengine muhimu kitaifa.
Katika mkutano huo ulifanyika uchaguzi wa viongozi
wapya wa tawi la JMAT Kagera ambao watakuwa na jukumu la kuongoza kwa kipindi
cha miaka mitatu (3). Uchaguzi huo ulifanyika kwa mujibu wa takwa la kikatiba kutokana
na uhamisho uliotokea kwa baadhi ya viongozi katika tawi hilo kwenda nje ya Mkoa
wa Kagera.
Nafasi ya Mwenyekiti ilichukuliwa na
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Bukoba, Mhe. Janeth Massesa, Makamu
Mwenyekiti aliyechaguliwa alikuwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Biharamulo Mjini,
Mhe Edward Samara.
Nafasi ya Katibu ilichukuliwa na Hakimu wa Mahakama ya Mwazo Bukoba Mjini, Mhe. Zakaria Nyahende, Mweka Hazina akachaguliwa Hakimu wa Mahakama ya Mwazo Nyaishozi, Mhe. Erasto Joseph, huku nafasi ya Mwakilishi wa JMAT Taifa ikichukuliwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Biharamulo, Mhe. Flora Ndale.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni