Jumatatu, 3 Oktoba 2022

JAJI MFAWIDHI SONGEA AWAPONGEZA WATUMISHI KWA MAHUSIANO MAZURI NA WADAU

Na Catherine Francis – Mahakama Kuu Songea

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Yose Mlyambina amewapongeza watumishi wa Mahakama Kanda ya Songea kwa kuwa na mahusiano mazuri na wadau wa Mahakama katika utekelezaji wa majukumu yo ya kila siku.

Mhe. Mlyambina alitoa pongezi hizo hivi karibuni wakati wa kikao cha menejementi cha robo ya kwanza ya mwaka 2022/2023. Jaji Mfawidhi huyo alisema kuwa amekuwa akishuhudia mahusiano hayo yakiimarika kila siku kwa Mahakama kushiriki katika matukio ya kijamii na ya kiserikali kama vile ushiriki kwenye sherehe za mbio za mwenge.

Alibainisha kuwa wadau mbalimbali wamekuwa wakishirikiana na Mahakama katika kutoa elimu ya sheria kwa jamii kwa kutumia njia kadhaakama vile redio zilizopo ndani ya Mkoa wa Ruvuma pamoja na kushirikiana katika michezo.

Kadhalika, Mhe. Mlyambina aliwapongeza Mahakimu ambao wameendelea kufanya kazi vizuri kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ya Mkoa wa Ruvuma, hivyo kufanikiwa kupunguza mashauri ya mlundikano kwa kiasi kikubwa kutoka 160 mwezi Januari hadi kufikia mashauri 14 mwezi Septemba. “Hii inaonyesha ni kwa namna gani tumekuwa mahusiano mazuri kati ya Mahakama na Taasisi nyingine,” alisema.

Vilevile Mhe. Mlyambina alisema kuwa ili kuweza kuendelea kudumisha mahusiano hayo mazuri ni vyema watumishi wa Mahakama Songea kujitafakari juu ya utendaji kazi wao, kwa kujipima wenyewe kama huduma wanayotoa kwa jamii zinaridhisha na pia wapate nafasi ya kujitathimini kama uwajibikaji wao ni wa uadilifu na unaofuata katiba ya nchi au wanafanya kazi kwa mazoea.

Jaji Mfawidhi huyo alisema kuwa kufanya hivyo kutapunguza malalamiko juu huduma zipatikanazo mahakamani na kurudisha imani kwa jamii yote kwa ujumla kwa kuwa Mahakama inafanya kazi kwa kufuata nguzo kuu tatu za Mpango Mkakati wa Mahakama na hii ikiwa Nguzo ya tatu, hivyo hawana budi kuendelea kuiboresha kila siku.

Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Yose Mlyambina (kushoto) ikifuatilia kikao kwa umakini. Wengine katika picha ni Jaji wa Mahakama Kuu Songea, Mhe. Upendo Madeha (kulia).
Baadhi ya wajumbe wa kikao wakifuatilia mada inayotolewa. Aliyesimama ni Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Mbinga, Mhe. Ally Mkama ambaye alikuwa akiwasilisha mada.

Picha ya pamoja kati ya meza kuu na wajumbe wa kikao.

(Picha na George Sabinus).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni