Ijumaa, 16 Juni 2023

MAJAJI WA RUFANI WADHIHIRISHA UTOAJI HAKI KWA WAKATI MKOANI KIGOMA


Na Aidan Robert- Mahakama, Kigoma

 

Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, limemaliza kusikiliza na mashauri 35 katika kikao cha Mahakama hiyo kilichoketi Mkoani Kigoma, kwa kipindi cha wiki tatu kuanzia tarehe 29, Mei 2023 mpaka tarehe 16 Juni, 2023.

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo tarehe 16 Juni, 2023 mjini Kigoma na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe.Dyness Lyimo imesema kikao hicho, kiliketi katika Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, ambapo jumla ya mashauri 30 yalipangwa kusikilizwa mbele ya jopo la Majaji hao kwa mchanganuo wa rufaa za madai 12, maombi ya madai sita, na rufaa za jinai 12.

 

Mhe. Dyness amefafanua kuwa kulikuwa na mashauri mengine matano yaliyopangwa kusikilizwa kwa faragha yenye mchanganuo wa maombi ya madai matatu, maombi ya jinai 2, na kusababisha jumla ya mashauri hayokufikia 35, ambayo yamesikilizwa kwa wakati na kutolewa uamuzi na Majaji hao.

 

“Majaji wa Mahakama hii ambao wamesikiliza mashauri hayo ni Mhe. Jaji, Stella Mugasha,(Mwenyekiti, Mhe. Jaji Barke Sehel, na Mhe.  Jaji Abrahaman Mwampashi ambao kwa hakika kazi wameifanya kwa weledi na ushirikiano mkubwa ili kufikia malengo ya kumaliza mashauri hayo kwa asilimia 100% na kwa muda uliopangwa,” amesema Mhe. Dyness.

 

Hata hivyo, ameongeza kwamba mkakati wa Majaji hao, wa kusikiliza mashauri matatu mpaka manne  kwa siku umezaa matunda na kufanikisha  mashauri yote kumalizika kwa wakati, ikiwa  ni sehemu ya utekelezaji wa  Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa Miaka Mitano( 2020/21- 20/24/25), nguzo ya pili ambayo inasema ‘Upatikanaji wa haki   kwa wakati’. 

 

Mhe. Dyness amesema mkakati huo, umeleta ufanisi wa kumaliza mashauri mengi zaidi katika kanda zote kwani Majaji wamejipanga vyema na kikazi  kuwapa Watanzania haki kwa wakati ili kuwawezesha wananchi waendelee na shughuli zao za kujenga uchumi wao na nchi bila kupoteza muda mahakamani. 

 


Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Barke Sehel, akiwa  ofisini kwake iliyopo Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, akijiandaa kwa ajili ya kikao cha hitimisho la kusikilizwa kwa mashauri.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dyness Lyimo, akiwa ofisini kwake akijiandaa kutoa taarifa ya hitimisho la vikao vya Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mkoani Kigoma.

Picha ya pamoja ya wasaidizi wa sheria wa Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania wakijiandaa na vikar hivyo.

Msaidizi wa Kumbukumbu na Nyaraka Mwandamizi Bw. Gerlad Ng’wandu, akiendelea na majukumu yake ya  kuhitimisha shughuli za vikao vya usikilizwaji wa mashauri katika masjala ndogo ya Mahakama ya Rufani Tanzania, iliyopo katika jingo la Mahakama Kuu ya  Tanzania Kanda ya Kigoma.

Baadhi ya wananchi waliokuwa ukumbini wakisubiri Mahakama  ya Rufani Tanzania kuanza kusikiliza mashauri yao katika ukumbi namba moja uliopo katika jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma.


(Picha na Aidan Robert- Mahakama, Kigoma)


(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni