Na Magreth Kinabo- Mahakama
Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) mkoa wa Dar es Salaam kimeandaa bonanza maalum kwa ajili ya kuendeleza michezo na shughuli za JMAT litakalofanyika tarehe 9 Septemba, 2023.
Akizungumza kikao cha viongozi wa JMAT wa mkoa huo tarehe 10, Agosti 2023 kwenye ukumbi wa maktaba ya Mahakama ya Tanzania, Mwenyekiti wa JMAT wa tawi la Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Shabani Lila amesema lengo la bonanza hilo ni kufahamiana, kuendeleza uhai wa chama hicho na kuamsha shughuli zake katika mkoa huo.
“Tuna rasilimali kubwa katika chama tunaweza kufanya mambo makubwa, tukianza na bonanza kwanza. Jambo linalotakiwa kufanywa sasa ni kuhamasisha wanachama ili waweze kushiriki,” amesema Mhe. Jaji Lila.
Ameongeza kwamba bonanza hilo litashirikia familia za wanachama hao na kuwaalika watumishi wa Mahakama ya Tanzania wa mkoa huo.
Naye Katibu wa JMAT wa tawi la Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Kifungu Mrisho, ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mwandamizi ametaja michezo itakayochezwa katika bonanza hilo ni mpira wa miguu na pete,kuvuta Kamba, kukimbiza kuku, kukimbia na gunia bao, kukimbia mita 100 na mita 400 na kuendesha baiskeli mwendo wa polepole.
Kikao hicho kimeshirikisha viongozi wa matawi matatu ya JMAT kutoka, Mahakama ya Rufani Tanzania, Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) wa tawi la Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Shabani Lila(kulia) akizungumzia kuhusu bonanza hilo. Kushoto ni Mwenyekiti wa JMAT tawi la Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, Mhe. Jaji Latifa Mansoor.
Makamu Mwenyekiti wa JMAT tawi la Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, Mhe. Mary Kallomo akichangia hoja.
Picha ya pamoja ya viongozi hao wa JMAT.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni