·Jaji Mfawidhi asisitiza kuienzi salamu ya Mahakama
Na Arapha Rusheke, Mahakama Kuu Dodoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma ambae pia ni Mlezi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzanua (JMAT) Tawi la Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Massabo amewasisitiza Viongozi na wanachama mkoani hapa kuhakikisha wanakutana mara kwa mara ili kuzidi kutambua changamoto mbalimbali za kikazi ili kuzitatua.
Mhe. Dkt. Massabo alitoa wito huo juzi tarehe 18 Novemba, 2023 alipokuwa anafungua mkutano wa chama hicho uliojumuisha Viongozi na wajumbe mbalimbali kwenye ukumbi wa Mahakama katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma.
“Niwapongeze wote kwa kazi kubwa ambayo mnafanya, kila mmoja kwa nafasi yake anatekeleza majukumu yake vizuri, hongereni sana. Lakini pia ninawashukuru kwa ushirikiano wenu kwani tangu nimefika hapa tarehe 2 Juni, 2023 mmekuwa na mimi bega kwa bega, naomba na kuwasihi muendelee na ushirikiano huu,” amesema.
Jaji Mfawidhi aliendelea kusisitiza, “JMAT ni sisi, JMAT sio Viongozi, kila mmoja wetu anawajibu wa kuhakikisha JMAT inafIkia malengo yake. Tushiriki katika shughuli za JMAT kama taratibu na miongozo ya chama inavyotutaka. Tuwe wabunifu, tubadilike.”
Aidha, Mhe. Dkt. Massabo aliwasihi na kuwaomba wanachama hao wa JMAT kuiishi salamu ya Mahakama ambayo inasema Uadilifu, Weledi Na Uwajibikaji,
kwani kwa kufanya hivyo wataishi vizuri na kuweza kutekeleza vyema majukumu yao nawasisitiza tuiishi hii salamu ya Mahakama na tusiisahau,” alisema.
Kikao hicho ni mwendelezo wa vikao ambavyo vimekuwa vikifanyika mara kwa mara katika kujengana uwezo na kujadili masuala mbalimbali wanayokutana nayo katika kazi zao na pia kupeana mbinu za kuzitatua changamoto hizo.
Wakati wa kikao hicho kuna mada ya moja inayohusu magonjwa na akili iliwasilishwa na Dakitari kutoka Hospital ya Taifa ya Milembe, Dkt. Mhando Kileo.
Baada ya kikao hicho kulifanyika uchaguzi wa Viongozi wa chama hicho ambapo Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kondoa, Mhe. Feisal Kahamba alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa JMAT Tawi la Dodoma, huku nafasi ya Mwenyekiti Msaidizi ikichukuliwa na Mhe. Deniss Mpelembwa na Mhe. Getrude Missana akiibuka kidedea kwenye nafasi ya Katibu.
Mkufunzi kutoka Hospital ya Taifa ya Mirembe Dkt. Mhando Kileo akitoa mada kwa wajumbe wa kikao hicho.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma (aliyesimama) ambaye pia ni Mlezi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) Tawi la Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Massabo akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa zamani wa JMAT Tawi la Dodoma. Kulia kwake aliyeketi ni aliyekuwa Mwenyekiti wa zamani wa JMAT Tawi la Dodoma Mhe. Sylvia Lushasi na kushoto kwake aliyekuwa Katibu Mhe. Deniss Mpelembwa.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni