Jumatano, 31 Januari 2024

MAHAKAMA, WADAU HAKI JINAI KIGOMA WATOA ELIMU KATIKA SHULE NA GEREZA

Na Aidan Robert, Mahakama Kigoma

Katika kuendelea na utoaji wa elimu wa makundi mbalimbali, Mahakama ya Tanzania Kanda ya Kigoma wametoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Buteko ambao wameipokea kwa shangwe.

Zoezi la utoaji wa elimu ya Sheria kwa wanafunzi hao lilifanyika tarehe 29 Januari, 2024 ambapo moja ya mambo waliyofurahishwa nayo ni pamoja na Salamu ya Mahakama ya Tanzania ambayo ni Uadilifu, Weledi, na Uwajibikaji.

Aidha, Maafisa kutoka Mahakama Kanda hiyo wakiwa wameambatana na Wadau wa Haki Jinai waliwajulisha wanafunzi hao kaulimbiu ya Wiki na Siku ya Sheria ya mwaka huu ambayo ni ‘Umuhimu Wa Dhana Ya Haki Kwa Ustawi Wa Taifa: Nafasi Ya Mahakama Na Wadau Katika Kuboresha Mfumo Jumuishi Wa Haki Jinai’

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Ujiji Kigoma, Mhe. Hassan Galiatano, ambaye aliambatana  wadau wa Mahakama mkoani humo waliongoza pia zoezi la utoaji elimu ya sheria katika Gereza la Bangwe Kigoma ambapo walifundisha juu ya muundo wa Mahakama na shughuli zake na kusema Mahakama ya mwanzo ndio Mahakama ya kwanza katika kupokea mashauri ya jinai na madai ya kawaida kutoka kwa jamii inayozunguka eneo hilo.

Hata hivyo, alisema baada ya hukumu ya Mahakama hiyo kutoka upande ambao haukuridhika na hukumu ipo nafasi ya kukata rufaa kwenda Mahakama ya Wilaya ili kuitafuta haki kwa upande usioridhika na maamuzi hayo Mpaka kufikia Mahakama ya rufani.

Amesema kuwa, Mahakama ya ngazi juu katika nchi yetu ni Mahakama ya Rufani ambayo kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu ndio yenye maamuzi ya mwisho katika kutoa haki nchini.

Amesema kwamba, Mahakama imefanya maboresho makubwa ya kiteknolojia katika silikiliza mashauri yaliyopo mahakamani ili kuwahisha haki kwa wananchi.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mashtaka, Bi. Edina Makala, amesema wanapopokea kesi kutoka Polisi na kuandaa mashtaka kwa ruhusa ya Mkurugenzi wa Mashtaka Taifa anaporidhia mtuhumiwa wa shtaka husika kushitakiwa Mahakamani, hapo ndio Mahakama huanza taratibu zake za kusikiliza shauri husika.

 Hata hivyo amebainisha kuwa, wao wanayo nafasi kubwa ya kuisaidia Mahakama kusikiliza kesi na kutoa hukumu kwa wakati kwani kufanya hivyo ndio jukumu lao la kila siku Mahakamani.

Aidha, kwa upande wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) mkoani hapa, Wakili Jemes Nyarobi, Afisa Uchunguzi akitoa elimu kwa wanafunzi na walimu wao amesema, Rushwa ni adui wa haki.

“Ninyi ni Taifa la kesho hivyo Taifa linawategemea, na kupitia maadhimisho haya tumekuja kuwafundisha kuwa pingeni rushwa na toeni taaarifa kwa mamlaka ili kuweza kukomesha vitendo vya rushwa mashuleni, mtaani na katika Taasisi za umma, ili kuwa na jamii yenye ustawi na kujali utu wa mtu katika kutoa huduma mbalimbali za umma bila aina yoyote ya rushwa,” alisema Wakili Nyarobi

Jeshi la Uhamiaji nalo halikubaki nyuma katika mnyororo wa haki jinai nao waliambatana na Mahakama katika kutoa elimu ya uhamiaji na uraia wa nchi na taratibu zake ili kujenga uelewa wa pamoja juu ya sheria zinazofanya kazi katika kuzuia uhamiaji haramu unaofanywa na watu mbalimbali kutoka nchi tofauti.

Afisa Uhamiaji, S/sgt. Mashaka Harun Kishaka, aliwataka wanafunzi na wazazi wao kutokubali kuishi na watu wasio wafahamu ambao baadae huleta madhara katika jamii, amesema Sheria inahitaji mhamiaji awe na vibali halali vya jeshi hilo ili kuishi nchini bila kupata shida ya aina yoyote, mbali na hapo amesema jeshi hilo litamkamata na kumshtaki mahakamani mtu yeyote asiye raia wa Tanzania.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Buteko, Bw. Hamad Mohamed alisema Elimu ya Sheria ni muhimu kwao na wanafunzi. Ameipongeza Mahakama na wadau wake kwa kuchagua Shule yao kwani zipo shule nyingi mkoani humo.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Ujiji Kigoma, Mhe. Hassan Galiatano (katikati) akiwa na wadau wa Haki Jinai wakijiandaa kwenda kutoa elimu ya Wiki ya Sheria katika maeneo mbalimbali ikiwemo shuleni.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Buteko, Bw. Hamad Mohamed (aliyesimama) akitoa neno la ukaribisho kwa watoa elimu ya Wiki ya Sheria wakiongozwa na  Mhe. Hassan Galiatano.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Ujiji Kigoma, Mhe. Hassan Galiatano (kushoto) akitoa zawadi kwa Mwanafunzi Juma Heri,  aliyejibu vizuri swali aliloulizwa na Hakimu huyo.

 Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Kigoma, Bi. Edina Makala akifafanua jambo wakati akitoa elimu ya sheria za jinai kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Buteko-Kigoma.
 Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Ujiji Kigoma, Mhe. Hassan Galiatano (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau, Walimu na Wanafunzi.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni