Alhamisi, 21 Machi 2024

JAJI MANSOOR AHIMIZA MATUMIZI YA TEHAMA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA

 ·       Tume Kutowavumilia Watumishi Walevi, Wazembe na Wabadhirifu

 Na Evelina Odemba na Lydia Churi – Mahakama Morogoro

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor ahimiza Tume ya Utumishi wa Mahakama kuendeleza matumizi ya Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kutekeleza majukumu yake.

Mhe. Mansoor aliyasema hayo wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama leo tarehe 20 Machi, 2024 kilichofanyika katika ukumbi wa Nashera ulioko Morogoro Mjini chini ya Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel.

Aidha Mhe. Mansoor alieleza kuwa Kwa kutumia TEHAMA, Tume  itarahisisha utendaji kazi, kupunguza gharama, kuokoa muda na kuongeza ufanisi wakati wa kutekeleza wa majukumu yake. Alitoa mifano mbalimbali ya namna ambavyo Tume imekuwa ikitumia mifumo ya TEHAMA katika utendaji kazi ikiwemo wakati wa kusaili watumishi walioomba nafasi mbalimbali za ajira ndani ya Mahakama.

 “Ni maelekezo ya Serikali kwa sasa juu ya matumizi ya TEHAMA, hivyo naipongeza Tume kwa kuweza kuanza kutumia mifumo ya TEHAMA, pia katika  michakato ya ajira tumeshuhudia ikifanyika kwa njia ya mtandao, haya ni mafanikio makubwa sana napongeza kwa jitihada hizi na nahimiza ziendelee zisiishie hapa”alisisitiza Mhe. Mansoor

Jaji Mansoor alitoa rai kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama kuendelea kusimamia rasilimali za Mahakama ikiwemo rasilimali watu ili kuweza kujenga Imani ya wananchi kwa Mahakama ya Tanzania. Pia aliwataka Watumishi kuwa waadilifu wanapotekeleza majukumu yao.

“Niwapongeze watumishi wa Tume hii kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuongoza, kusimamia, kushauri na kufuatilia utekelezaji wa Shughuli za Tume na Mahakama ya Tanzania” alisema Mhe. Mansoor.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kuwa Tume ina jukumu kubwa la kuisimamia Mahakama ya Tanzania ili kuongeza imani ya wananchi na wadau kwa Mhimili huo.

Alisema kutokana na usimamizi mzuri wa maadili ya watumishi, imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama imeongezeka kutoka asilimia 78 mwaka 2019 na kufikia asilimia 88 mwaka 2023.

’’Pamoja na mafanikio haya mazuri tuliyoyapata, Tume haitamvumilia mtumishi yeyote atakayejishirikisha na vitendo vinavyokiuka maadili katika kazi. Sitawavumilia watumishi walevi, wazembe na wabadhirifu wa mali za Umma”, alisema Katibu huyo wa Tume.

Akizungumzia matumizi ya TEHAMA, Prof. Ole Gabriel alisema Tume imekuwa ni Taasisi ya kwanza katika matumizi ya Tehama kwenbye usaili. Alisema wamekuwa wa kwanza kubuni utaratibu wa kutumia TEHAMA katika usaili wa awali yaani kabla ya Msailiwa kufika kwenye hatua ya mahojiano ya ana kwa ana (Oral Interview).

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Tume imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama jana mkoani Morogoro.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama jana mkoani Morogoro.
Sehemu ya Watumishi wa Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama wakifuatilia Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi jana mkoani Morogoro.


Manaibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wakiwa kwenye Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi jana mkoani Morogoro. Kulia ni Naibu Katibu wa Tume (Ajira) Bi. Enziel Mtei na kushoto ni Naibu Katibu wa Tume (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Mbuya.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa TUGHE mara baada ya kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi jana mkoani Morogoro.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Tume Wanawake mara baada ya kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi jana mkoani Morogoro.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Tume Wanaume mara baada ya kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi jana mkoani Morogoro.












Hakuna maoni:

Chapisha Maoni