· Kamati yaishauri Serikali kumsimamia Mkandarasi kwa ukaribu zaidi
· Yashangazwa na kasi ndogo ya utekelezwaji wa mradi na kutoa maelekezo kwa Serikali
Na Innocent Kansha – Mahakama, Songea
Kamati Maalumu ya Bunge ya Katiba na Sheria jana tarehe 14 Machi, 2024 ilikagua Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kinachojengwa Songea mkoani Ruvuma chenye thamani ya shilingi takribani Bilioni 10.
Akizungumza wakati wa zoezi la ukaguzi wa ujenzi wa Kituo hicho Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Muhagama alisema Mradi huo ni moja ya Miradi mikubwa inayotekelezwa nchini kupitia Wizara ya Katiba na Sheria na mtekelezaji ni Mahakama ya Tanzania.
“Mradi huu upo nyuma sana asilimia tatu ya utekekelezaji wake hairidhishi hata kidogo kulinganisha na Miradi mingine ya Mahakama tuliyoikagua. Maagizo ya Kamati inamuagiza Mkandarasi kupiga kambi eneo la utekelezaji wa mradi na kuendesha ujenzi usiku na mchana ili kuweza kuendana na muda wa mkataba kwani inaonesha imesalia miezi 6 tu kulingana na Mkataba wa ujenzi,” alisema Mhe. Dkt. Muhagama.
Mwenyekiti huyo aliielekeza Wizara ya Katiba na Sheria kufanya ufuatiliaji wa karibu wa Mradi huo. “Kama Mradi huu utaendelea kusuasua tunaweza kuishauri Serikali imuondoe Mkandarasi muda wowote wakati wa utekelezaji wa ujenzi wa mradi ikiwa mkandarasi aliyepewa kazi haendani na kasi ya Mhe. Rais na kama maendeleo ya Mradi hayatakuwa yanaridhisha tutaishauri Serikali ichukue hatua zingine,” alisistiza Mwenyekiti.
Mhe. Dkt. Muhangama aliongeza kuwa, Kamati imefuatilia suala la ongezeko la thamani (VAT) katika utekelezaji wa Miradi ya Mahakama na kujiridhisha kwamba siyo kikwazo cha ucheleweshaji wa Mradi. Kuna Miradi iliyokwishaombewa msamaha wa ongezeko la thamani hali kadhalika vifaa vya ujenzi vilivyoombewa msamaha wa kodi miradi hiyo imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wake mathalani Mradi wa Njombe.
“Niwaombe Wakandarasi muombe hiyo misamaha ya kodi kwa wakati kwani maombi haya yote yanafanyika kidijitali na watu wa Mahakama wapo kwa ajili yenu kuhakikisha mambo yote yanaenda kwa wakati, hivyo kama kuna ucheleweshaji wowote wa utekelezaji wa Mradi Kamati itajua ni Mkandarasi na si vinginevyo,” alisisitiza Mwenyekiti wa Kamati.
Kamati
hiyo maalum imeahidi kurudi kukagua mradi huo kabla ya kupitisha bajeti ya
Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
“Niwaombe Serikali msibweteke mkadhani kwamba baada ya kumwezesha Mkandarasi kazi hii ya utekelezaji wa Mradi itaendelea bila kumsimamia Mkandarasi kwa ukaribu zaidi tumeona maendeleo ya mradi sehemu nyingine yanaridhisha lakini hapa Songea kasi ya utekelezaji ni ndogo sana,” alisema Mwenyekiti kwa niaba ya Kamati.
Mhe.
Dkt. Muhagama aliongeza kwamba, kumuondoa Mkandarasi mzembe kazini bila kumdai fidia za ucheleweshaji
na usumbufu nchi haiwezi kwenda hiyo aliwataka wakandarasi kujipanga na
kutekeleza Miradi kwa wakati kama ilivyokusudiwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana aliishukuru Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa kuendelea kutembelea miradi yote iliyopo chini ya Wizara, “huu ni moja ya Mradi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki unaoendelea kutekelezwa mkoani Ruvuma na maoni ya Kamati kwa Mkandarasi yamekwisha kutolewa hivyo imebaki utekelezaji bila kuchelewa,” alisema Mhe. Dkt. Chana.
“Kwa kweli Mkandarasi inakupasa ujitahidi ili kuendana na wakati, hii ni Miradi ya Serikali na ni Vituo vya kutoa huduma kwa wananchi, kwa hiyo kimsingi lazima yale makubaliano tuliyowekeana ifikapo mwezi wa 9 mwaka huu ujenzi wa Mradi huu uwe umekamilika hakuna namna yanaweza kukiukwa baina ya pande zote mbili,” alisisitiza Waziri huyo.
Aliongeza kwa kumtaka Mkandarasi huyo kufanya kazi bila kuchoka ili kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri na hatimaye kukamilisha Mradi huo ulioshuhudiwa na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria.
Aidha, Mhe. Dkt. Pindi Chana alitoa wito kwa Mkandarasi anayetekeleza Mradi huo kwamba endapo kuna changamoto zozote milango ya Serikali ipo wazi kueleza changamoto ni nini na ugumu unatoka wapi katika utekelezaji wa Mradi ili Serikali izitatue kwa haraka bila kuchelewesha badala ya kuambiana changamoto wakati wa ukaguzi.
“Miradi hii inatumia pesa za umma kwa hivyo ni lazima tuzisimamie vizuri mchakato wake wakati mradi unapotekelezwa ili kuonesha uhalisia na thamani yake,” alisema Waziri Chana.
Mhe.
Dkt. Chana alisema, azma ya ukaguzi huo wa Kamati Maalum ya Bunge ya Katiba
na Sheria unaenda sambamba na maelekezo ya Rais Samia ya kuboresha miundombinu
ya utoaji haki kwa maana ya “Reforms & Rebuilding” ili watanzania wote
wapate haki kwa usawa na kwa wakati kama ilivyokusudiwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni