Alhamisi, 30 Mei 2024

KILA MTUMISHI MAHAKAMANI ANALAZIMIKA KUJUA MATUMIZI YA TEHAMA: JAJI KIONGOZI

Na Lusako Mwang’onda-Mahakama Kuu, Iringa

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustafa Mohamed Siyani amewahimiza Watumishi wa Mahakama kujielekeza katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Maasiliano (TEHAMA) ili kwenda sambamba na maboresho mbalimbali yanayoendelea sasa katika Mahakama ya Tanzania. 

Mhe. Siyani ametoa wito huo leo tarehe 30 Mei, 2024 alipokuwa anazungumza na Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa.

Amesisitiza kuwa hakuna namna yoyote kwa sasa mtumishi wa Mahakama kutoka Kada yoyote anaweza kufanya kazi mahakamani pasipokuwa na uelewa wa msingi katika masuala ya TEHAMA. 

“Kwa sasa Mahakama yetu inaendelea kufanya maboresho mbalimbali ya kiutendaji, maboresho ambayo yanamlazimisha kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anakuwa na ujuzi wa matumizi ya TEHAMA,” Mhe. Siyani amesema.

Pamoja na kuweka msimamo huo, Jaji Kiongozi amesisitiza nidhamu kazini, uadilifu katika utumishi, weledi kazini, utunzaji wa mazingira na mazoezi kwa ajili ya kuimarisha afya.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustafa Mohamed Siyani akisisitiza jambo wakati akizungumza na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustafa Mohamed Siyani (katikati) akiwa pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa. Kulia kwake ni Jaji MfawidhiMhe. Ilvin Mugeta na Mhe. Angaza Mwipopo na kushoto kwake ni Mhe. Said Kalunde na Mhe. Dkt. Eliamani Laltaika.

Sehemu ya umati wa watumishi wa Mahakama Kuu Iringa wakimsikiliza kwa makini Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustafa Mohamed Siyani (hayupo pichani).


 Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Dkt. Eliaman Laltaika (aliyesimama) akiwasilisha neno la shukrani kwa Jaji Kiongozi kwa niaba ya watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Iringa.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni