Na Aidan Robert, Mahakama Kigoma
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe.Rose Kangwa leo tarehe 29 Mei, 2024 amekabidhiwa Mwongozo wa Rufaa kwa Manusura wa Ukatili wa Kijinsia Mkoa wa Kigoma kutoka Shirika la Kimataifa la Uokoaji wa Jamii (IRC).
Akizungumza kwa niaba ya Wadau wote waliokabidhiwa Mwongozo huo alipokuwa akiongoza kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Kigoma leo, Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Kangwa amesema, “Mwongozo huu utasaidia utoaji wa huduma za msaada wa Kisheria kwa Wadau ambao wanashughulikia manusura wa ukatili wa kijinsia ili kukuza na kusaidia wahanga kujua haki zao na katika kushughukikia upatikanaji wa haki na kufanya maamuzi sahihi kuhusu haki zao.”
Aidha, Mfawidhi huyo amesema kuwa, Mwongozo huo umekuja muda muafaka, kwakuwa utawezesha wadau kuelewa vema jukumu lao la msingi katika kushughulikia manusura wa ukatili wa kijinsia katika maeneo yao na namna ya kuweza kuwasaidia manusara hao kulinda haki zao katika jamii husika.
Naye, Afisa kutoka Shirika la Kimataifa la Uokoaji wa Jamii (IRC), Bi. Marcela Sulley amesema, “lengo la kukabidhi Mwongozo wa Rufaa kwa Manusura wa Ukatili wa Kijinsia kwa Mkoa wa Kigoma ni kurahisisha mawasiliano kwa watoa huduma wa manusura wa ukatili wa kijinsia katika Halmashauri zote ndani ya Mkoa wa Kigoma.”
Walioshiriki katika zoezi la kukabidhiwa Mwongozo huo pamoja Mahakama ni Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Polisi Dawati Mkoa, Ofisi ya Maendeleo ya Jamii na Ofisi ya Ustawi wa Jamii Kigoma.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe.Rose Kangwa (aliyeketi mbele) akiongoza kikao kilichohudhuriwa na Wadau kadhau mara baada ya kukabidhiwa Kitabu cha Mwongozo wa Rufaa kwa Manusura wa Ukatili wa Kijinsia kutoka kwa Afisa kutoka Shirika la Kimataifa la Uokoaji wa Jamii (IRC).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni