Na FAUSTINE KAPAMA -Mahakama, Dar es Salaam
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Dar-es-Salaam, leo tarehe1Mei, 2024 wameungana na Watanzania wengine kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi, inayojulikana kama Mei Mosi, inayosherekewa kote duniani.
Maadhimisho hayo ambayo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila yamefanyika katika Uwanja vya Uhuru jijini hapo na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi.
Pilikapilika za maadhimisho hayo zilianza mapema asubuhi ambapo watumishi wa Mahakama waliojitokeza kwa wingi waliungana na wananchi wengine katika eneo la Mnazi Mmoja na baadaye kushiriki kwenye maandamano hadi kwenye Uwanja wa Uhuru.
Maandamano hayo yaliyoongozwa na Bendi ya Jeshi la Magereza yalipita katika barabara ya Nyerere, Keko na baadaye Uwanja wa Uhuru na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa.
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania ndiyo waliokuwa wa kwanza kuingia katika Uwanja wa Uhuru na kushangiliwa kwa nguvu na wananchi waliofurika uwanjani hapo kufuatia kazi nzuri wanayoifanya katika muktadha mzima wa utoaji haki nchini.
Mhe. Chalamila aliongoza jukwaa kuu kuwashangilia watumishi wa Mahakama walipokuwa wanapita mbele yake na kupokewa na wananchi wengine waliokuwa wamesimama muda wote.
Mbali na watumishi kupita mbele ya mgeni rasmi kwenye maandamano hayo, magari ya Mahakama nayo yalikuwa miongoni kutoka Taasisi na mashirika mbalimbali ambayo yalipita mbele yake, likiwemo gari la Mahakama Inayotembea, ‘Mobile Court’, ambalo lilikuwa kivutio kikubwa kwa wananchi.
Baada ya maandamano hayo, ratiba ya maadhimisho hayo iliendelea, ikiwemo viongozi mbalimbali wa Chama cha Wafanyakazi (TUCTA) na Serikali ya Mkoa walipata nafasi ya kutoa salamu.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Chalamila amewapongeza wafanyakaizi wote kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye maadhimisho hayo ambayo kwa mwaka huu wa 2024 yamebeba kauli mbiu inayosema, “Nyongeza ya mishahara ni msingi wa mafao bora na kinda dhidi yahali ngumu ya maisha.”
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Dar-es-Salaam wakijiandaa kushiriki katika maandamano kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani.
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Dar-es-Salaam wakiingia kwenye Uwanja wa Uhuru kushiriki katika maandamano kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani.
Safari kuelekea katika maeneo ya Mnazi Mmoja ndiyo inaanza kushiriki katika maandamano ya kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani.
Sehemu ya magari ya Mahakama ya Tanzania yakiwa yamefurika watumishi yakiwasili katika maeneo ya Mnazi Mmoja kabla ya kuanza maandamano hayo.
Maandamano yameanzia sasa.
Maandamano yamekolea....
Wananchi wakiimba wimbo wa mshikamano katika Uwanja wa Uhuru baada ya maandamano.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni