Na IMAN MZUMBWE- Mahakama, Songwe
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Beda Ndunguru jana tarehe 13 Juni, 2024 alifanya ziara ya ukaguzi wa Mahakama ya Wilaya ya Ileje na Mahakama ya Mwanzo
Itumba zilizopo mkoani Songwe kwa lengo la kufanya ufuatiliaji wa utendaji kazi
za kimahakama.
Katika
ziara hiyo Mhe. Ndunguru alipata wasaa wa kuitembelea Mahakama ya Mwanzo Itumba
na kufanya ukagua wa Mahakama hiyo, vilevile alikukutana na wananchi waliokuwa
wamefika mahakamani hapo kupata huduma mbalimbali za kimahakama na kuzungumza
nao.
Akisikiliza
sehemu ya kero za wananchi hao Mhe. Ndunguru alikutana na Bw. Imani Bughi na
Bi. Rhoda Kamwela waliofika mahakamani hapo kwa shauri la Talaka, mara baada ya
kuzungumza nao kwa kina, alifanikiwa kuwapatanisha wadaawa hao wa shauri la
Talaka kwa njia ya usuluhishi.
Jaji
Ndunguru aliwasihi wanandoa hao kumaliza tofauti zao kwani bado wana mtoto
mchanga amabaye anahitaji malezi ya wazazi wote wawili. Wanandoa hao wawili
waliridhia kwa kusema kuwa wapo tayari kusameheana, kurudiana na kuishi pamoja
kama mwanzo kwa maslahi ya ustawi wa familia yao.
Akizungumza
wakati wa Kikao na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Ileje na Mahakama ya Mwanzo
Itumba Mhe. Ndunguru aliwapongeza watumishi hao kwa kazi nzuri wanayoifanya
hasa katika eneo la usikilizaji na umalizaji wa mashauri.
“Nichukue
nafasi hii kuwasisitiza watumishi kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili
kuongeza ufanisi katika uwajibikaji wetu tunapowahudumia wananchi, kwa kufanya
hivyo tutakuwa tumewajengea wananchi imani kubwa tunapotoa haki,” aliongeza
Jaji Ndunguru.
Aidha,
Mhe. Ndunguru aliwapongeza watumishi wa Mahakama hiyo kwa kuanzisha Chama cha
kusaidiana na kuwaahidi kuwachangia kiasi cha shilingi 200,000/- kama motisha kwa
kuonesha ubunifu. Chama hicho hutoa mikopo midogodogo kwa watumishi ili
kukabiliana na changamoto za kimaisha.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Beda Ndunguru akisaini Kitabu cha Wageni alipowasili Mahakama ya Wilaya Ileje kufanya ziara ya ukaguzi wa shughuli za Mahakama jana tarehe 13 Juni, 2024.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Beda Ndunguru (Mwenye suti ya Dark Bluu) akisalimiana na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Ileje alipofanya ziara ya ukaguzi wa shughuli za Mahakama.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Beda Ndunguru na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Bi. Marvis Miti wakizungumza na wananchi waliokuwa wamefika Mahakama ya Mwanzo Itumba kwa ajili kupata huduma.
Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu akizungumza na waliokuwa wadaawa wa shauri la talaka, Bw. Imani Bughi na Bi. Rhoda Kamwela, wanandoa hao waliokubali kurudiana mara ya baada ya kusuluhishwa na kufikia maridhiano ya kuendelea kuishi pamoja.
(Habari Hii Imehariri na Innocent Kansha-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni