Jumamosi, 29 Juni 2024

KAMA HUJARIDHISHWA NA UAMUZI USIKATE TAMAA BALI KATA RUFAA - JAJI MBAGWA

Na Eunice Lugiana,  Mahakama-Pwani

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Awamu Mbagwa ametoa rai kwa mahabusu na wafungwa wa Gereza la Mkuza lililopo mkoani Pwani kutokata tamaa wanaposhindwa katika shauri badala yake wanatakiwa kukata rufaa.

Mhe. Mbagwa aliyasema hayo jana tarehe 28 Juni, 2024 alipotembelea katika Gereza la Mahabusu la Mkuza lililopo mkoani Pwani kwa ajili ya kufanya ukaguzi katika Gereza hilo. 

Akizungumza na wafungwa na mahabusu katika Gereza hilo  ambapo wafungwa wengi walionekana kutoridhishwa na hukumu za vifungo walizopewa na Mahakama  na kuendelea kukaa kimya  na kuonekana wamekata tamaa wakati hawajaridhika na adhabu hizo. Mhe. Mbagwa alisema “pale maamuzi yanapotolewa katika Mahakama kama hujaridhika na maamuzi hayo usikate tamaa badala yake kata rufaa katika Mahakama ya juu.”

Aidha, Mhe.Mbagwa aliwaomba Mahakimu kutofurahia kuwa na mahabusu wengi ambao makosa yao yanadhaminika bali wajitahidi kuwaelimisha washtakiwa kutafuta wadhamini ili kupunguza msongamano katika Gereza hilo. 

Mkuu wa Gereza hilo, Mrakibu wa Magereza Ibrahim Nyamka  alimueleza Jaji Mbagwa changamoto wanazokumbana nazo katika kusafirisha mahabusu kwenda magereza kuwa, ni pamoja na ukosefu wa magari ya kubebea mahabusu kupeleka mahakamani na wakati mwingine kulazimika kutofika mahamakani. 

Hata hivyo, alisema kwa mwaka ujao wa fedha 2024/2025 wameahidiwa kupatiwa basi la kubeba mahabusu na kusema kwamba, hatua hiyo itasaidia kuondoa usumbufu wa kutofika mahakamani kwa mahabusu.

Kadhalika, Mrakibu huyo aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha vijijini kuwapatia eneo la kujenga Gereza ili kuweza kuwafikia mahabusu wanaohudhuria Mahakama za pembezoni kama Soga na Magindu.

Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mlandizi, Mhe. Joseph Luoga alisema kuhusu hoja ya mahabusu kutofika mahakamani kwa changamoto ya usafiri, aliomba Magereza na wadau wengine wa haki jinai kuingia katika mfumo ili kuweza kuendana na teknolojia iliyopo ya mifumo kama ilivyo kwa Mahakama na kuongeza kuwa.

Mhe. Luoga aliongeza kuwa, hatua hiyo itaondoa usumbufu na kupunguza gharama za kusafirisha mahabusu na kuokoa muda wa kusafiri kupeleka mahabusu. 

Alisema mifumo ikisomana itakuwa rahisi hata kusikiliza shauri bila mtu kusafiri anasikiliza akiwa gerezani huku akiongeza kuwa, Mahakama iko mbele ki TEHAMA.

Naye, Mrakibu wa Polisi, Mganga Madali alisema kwamba, kuna tatizo la kutoingia kwenye mfumo kwa kuwa hakuna mkongo wa Taifa.

Upande wa Ofisi ya Mashtaka ya Taifa, wanao mfumo unaosomana na mfumo wa Mahakama lakini hausomani na wadau wengine.

Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Amina Macha alisema wametuma maombi Makao Makuu Dodoma ili kufanya mfumo wao usomane na wadau wengine ili waone mwenendo mzima wa shauri ili wasipoteze tarehe za kuita mashahidi. 

Aliongeza kwamba, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa pia wameanza mafunzo ya namna ya kutumia mfumo mara tu wamalizapo watakua ni sehemu ya mfumo huo.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Bi. Matilda Zakaria alitoa maoni yake mbele ya Jaji Mbagwa kuhusu Sheria ya Mtoto kwamba imepitwa na wakati maana mtoto wa miaka 17 kwa karne hii ni mtu mzima hivyo kutokana na Sheria kuwa rafiki kwake amekua akifanya kosa akijua kabisa adhabu yake ni ndogo na sio kifungo.

Akizungumza kuhusu suala hili, Mhe.Mbagwa alisema sheria imekuja ili kuweka nafuu (mitigate) kati ya ubinadamu na haki huku akitoa mfano kwa kusema kuwa, kwa kawaida katika ubinadamu binti wa miaka 17 na kijana wa miaka 19 binti anakuwa mkubwa ki akili hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kwamba binti anaweza kuwa amemshawishi kijana lakini sheria inamtambua binti kama ni mtoto na kijana ni mtu mzima.

Katika ziara hiyo, Jaji Mbagwa aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Livin Lyakinana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi, Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Fahamu Kibona, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Mwanzo Mailimoja, Mkuza na Mlandizi pamoja na wadau wa haki jinai wa Mkoa wa Pwani.

Jaji wa Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Awamu Mbagwa (mwenye suti nyeusi) akisalimiana na Askari Magereza baada ya kuwasili katika Gereza la Mkuza Mkoa wa Pwani kwa ziara ya ukaguzi. Nyuma yake ni Mkuu wa Gereza hilo Mrakibu wa Magereza Ibrahim Nyamka.

Jaji Awamu Mbagwa (wa pili kulia) akipokea taarifa ya awali kutoka kwa Mkuu wa Gereza  Mrakibu wa Magereza Ibrahimu Nyamka (wa kwanza kulia)  baada ya kuingia mapokezi. Wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Livin Lyakinana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama na wadau wengine walioambatana na Jaji Mbagwa katika ziara yake kwenye Gereza la Mahabusu na Wafungwa la Mkuza mkoani Pwani.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Awamu Mbagwa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama pamoja na wadau. Kutoka kulia ni Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Matilda Zakaria, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Livin Lyakinana. kutoka kushoto ni  Mkuu wa Gereza la Mkuza Mrakibu wa Magereza Ibrahimu Nyamka na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi. 

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni