Alhamisi, 27 Juni 2024

KONGAMANO LA KIMATAIFA LA MAHAKAMA KUHUSU MILIKI BUNIFU LAPAMBA MOTO

Na FAUSTINE KAPAMA -Mahakama, Dar es Salaam

 

Kongamano la Kimataifa la Mahakama kuhusu Haki Miliki, Alama za Biashara na Usimamizi wa Mashauri, ambalo limeandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) limeingia siku ya pili leo tarehe 27 Juni, 2024.

 

Katika siku ya pili asubuhi ya Kongamano hilo, Majaji wa Tanzania, Majaji kutoka Mahakama ya Uingereza na Kenya, Naibu Wasajili na Mahakimu wa Mahakama ya Tanzania wamepitishwa katika mada mbalimbali kuwajengea uwezo katika kushughulikia mashauri yanayohusu miliki bunifu.

 

Naibu Jaji wa Mahakama Kuu ya Uingereza, Mhe. Daniel Alexander alikuwa wa kwanza kutoa mada kuhusu mahitaji ya kiushahidi, akifuatiwa na Mwanasheria kutoka Taasisi ya Mahakama ya WIPO, Geneva Uswisi, Bi Ines Fernandez Ulate, ambaye aliwasilisha mada inayohusiana na ushahidi wa kidijitali katika mashauri ya alama za biashara. 

 

Mtoa mada wa tatu wakati wa kongamano hilo alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Kenya, Mhe. Francis Tuiyott, ambaye mada yake ilijikita katika hatua za nafuu za dharura katika madai na jinai.

 

Jana tarehe 26 Juni, 2024, Mratibu wa WIPO na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Upendo Ngitiri aliwasilisha mada kuhusu hali ya uendeshaji wa mashauri ya miliki bunifu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.      

 

Alilieleza kuwa hivi karibuni kuna ongezeko kubwa la mashauri yanayohusu miliki bunifu hususan yale yanayohusu uvunjifu wa miliki bunifu na alama za biashara. 

 

Alitoa mifano mbalimbali ya kesi zilizoamuliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama ya Rufaa na kueleza kuwa Mahakama kupitia maamuzi inayotoa ina mchango mkubwa katika kulinda miliki bunifu. 

Kongamano hilo lilifunguliwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambaye aliwataka Majaji na Mahakimu kusimamia masuala ya haki miliki kwa haki na ufanisi katika robo ya pili ya karne ya 21.

"Sote tunakubali kwamba Karne ya 21 inakwenda kwa kasi,na mipaka mingi mipya inayohitaji Mahakama kushika kasi. Hakuna shaka kwamba, katika miaka ijayo, mashauri ya haki miliki yataendelea kuvuka mipaka mipya,” alisema.

Jaji Mkuu alisema kwamba kutokana na mabadiliko ya haraka ya teknolojia ya kisasa na akili bandia, robo ya pili ya Karne ya 21 itashuhudia ubunifu na uvumbuzi wa kuvuka mipaka. 

 

Mahakama ya Tanzania na Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) kwa pamoja walisaini hati ya makubaliano tarehe 5 Machi, 2021 kwa madhumuni ya kushirikiana katika maeneo mbalimbali yaliyolenga kuboresha utoaji haki kwenye eneo la miliki bunifu “Intellectual Property” na usuluhishi wa migogoro mahakamani.

 

WIPO imekuwa ikishirikina na Mahakama ya Tanzania katika maeneo mbalimbali ambayo yamelenga kuboresha utoaji haki katika eneo la miliki bunifu kwa zaidi ya miaka mitano. 

 

Kwa kipindi cha miaka mitano Mahakama ya Tanzania, imepiga hatua kubwa katika kuboresha utoaji haki katika eneo la mashauri yanayohusu Miliki Bunifu kwa kushirikiana na Shirika la Miliki Bunifu Duniani ‘World Intellectual Property Organisation (WIPO)’.  

 

Miongoni mwa mafanikio yanayotokana na ushirikiano huo ni pamoja na kuandaa miongozo juu ya haki miliki (Copyright), alama za biashara (trademarks), hataza (patent) na maumbo bunifu (Industrial design). Miongozo hiyo inatumiwa na waheshimiwa Majaji na Mahakimu kama rejea pale wanapokuwa wanaendesha na mashauri yanayohusu miliki ubunifu.  

 

Kuanzia mwaka 2022 hadi 2023 Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) lilitoa ufadhili kwa Majaji na Mahakimu 250 kwa lengo la kusoma masomo hayo kwa njia ya masafa ‘Distance Learning Course’. Mafunzo hayo ya masafa yameongeza uelewa mkubwa kwa washiriki, hususani katika eneo la miliki ubunifu.

 

Jambo hili linadhihirisha kuwa Mahakama ya Tanzania hivi sasa ina Majaji na Mahakimu wengi waliobobea kwenye eneo hili na wameiva katika kutoa huduma bora kwa mashauri yanayohusu miliki ubunifu.

Mratibu wa Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Upendo Ngitiri akiwasilisha mada kwenye Kongamano la Kimataifa la Mahakama kuhusu Haki Miliki, Alama za Biashara na Usimamizi wa Mashauri linalofanyika jijini Dar es Salaam.

Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Kenya, Mhe. Francis Tuiyott akisisitiza jambo wakati anawasilisha mada kwenye Kongamano hilo.

Naibu Jaji wa Mahakama Kuu ya Uingereza, Mhe. Daniel Alexander akiwasilisha mada wakati wa Kongamano.


Mwanasheria kutoka Taasisi ya Mahakama ya WIPO, Geneva Uswisi, Bi Ines Fernandez Ulate, akiwasilisha mada inayohusiana na ushahidi wa kidijitali katika mashauri ya alama za biashara. 

 


Majaji wa Mahakama ya Rufani (juu) na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania (chini) wakifuatilia uwasilishaji wa mada hizo.






Sehemu ya Naibu Wasajili na Mahakimu wa Mahakama ya Tanzania (picha tatu juu na picha tatu  chini) wakiwa katika Kongamano hilo.









Hakuna maoni:

Chapisha Maoni