Jumanne, 25 Juni 2024

MAHAKAMA YA MWANZO MATIRI YAZINDULIWA

Na NOEL SYLIVESTER – Mahakama, Songea

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha, tarehe 21 Juni, 2024 alizindua jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo Matiri lililopo katika Kata ya Matiri, Tarafa ya Kigonsera na Wilaya ya Mbinga, kwa ajili ya utoaji wa huduma za kimahakama.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzio huo, Mhe. Karayemaha aliwapa pole wakazi wa Kata ya Matiri walioteseka kutokana na umbali wa kutafutaji wa haki zao na kupelekea wengine kukosa haki zao, kwani awali wananchi walilazimika kusafiri zaidi ya umbali wa kilomita 35 kufuata huduma za Mahakama ya Mwanzo.

“Niwape pole wakazi wa kata hii kwa kipindi cha nyuma kabla ya kuanzishwa kwa Mahakamna hii ya Mwanzo Matiri ambapo mlikuwa mnasafiri kwa umbali kufuata huduma za Mahakama ya Mwanzo Rwanda, wengine Litembo na Kigonsera. Wengine walikosa haki zao kwa kushindwa kusafiri kwa kukosa kumudu gharama za kujikimu,” alisema.

Jaji Mfawidhi alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kutumia Mhimili wa Mahakama kupata haki zao badala ya kwenda kwenye Mahakama zisizo rasmi kwani, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 107A, Mahakama ndio Taasisi pekee iliyopewa jukumu la kutoa haki.

“Ndugu wageni waalikwa, natambua kuna Mahakama nyingi mtaani, lakini nchi yetu inaongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na kwa mujibu wa Ibara ya 107A, Mahakama ndio Mhimili uliopewa jukumu la kutoa haki. Hvyo wanachi wenzangu tutumie Mahakama iliyopewa jukumu kikatiba na kuepuka kutumia njia isiyo rasmi,” alisema.

Alitoa rai kwa Viongozi wote wa Mahakama kuhakikisha kwamba watumishi wote wa Mahakama wanatoa huduma nzuri zinazoendana na uzuri wa jengo, bila kusahau kubadili mienendo na tabia ambazo zinakiuka miiko na maadili ya kazi kwa watumishi wa umma.

“Natoa rai kwa Viongozi wote wa Mahakama, majengo haya ya kisasa na miundombinu yake ni bora na mizuri, hivyo mnapaswa kuhakikisha watumishi wote wanatoa huduma nzuri zinazoendana na uzuri na obora wa jengo, na kubadili mienendo na tabia ambazo zinakiuka miiko na maadili ya kazi kwa watumishi wa umma,” alisema.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (wanne kutoka kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Matiri.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha akihutubia mbele ya wageni waalikwa na watumishi wa Mahakama Kanda ya Songea (picha chini).

 Sehemu ya wananchi wa Kata ya Matiri wakifatilia kwa karibu hotuba ya mgeni rasmi ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (hayupo kwenye picha). 
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni