Jumatatu, 10 Juni 2024

MKUU WA WILAYA BUSEGA AMALIZA MGOGORO WA MIPAKA MAHAKAMA YA MWANZO NYASHIMO

Na Naumi Shekilindi-Mahakama, Simiyu

Mgogoro wa mipaka uliodumu kwa takribani miaka 12 kati ya Mahakama ya Mwanzo Nyashimo na Ofisi ya Afisa Tarafa Nyashimo umemalizika baada ya Mkuu wa Wilaya Busega, Bi. Faidha Suleiman kuingilia kati.

Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita ndiye mwanzilishi wa kuomba maridhiano ili kutatua mgogoro huo uliosababishwa na kukosekana kwa ramani ya eneo hilo na hivyo kuleta mabishano ya mipaka kati ya ofisi hizo mbili.

Bw. Kanyairita alimuomba Mkuu wa Wilaya kufika katika eneo la tukio na wataalamu wa ardhi ili kwa pamoja waweze kufikia muafaka wa mgogoro huo.

Mhe Faidha alitoa maagizo kwa Afisa Ardhi kumpatia mchoro mpya wa eneo hilo kutokana na makubaliano yaliyofanyika.

Aidha, Mkuu wa Wilaya aliwaelekeza Viongozi waliokuwepo, akiwemo Afisa Tarafa na Afisa Ardhi Bw. Martin kufanya kazi kwa haraka na kwa usahihi ili kuepusha migogoro ya ardhi, hivyo kuiwezesha Mahakama kufanya maboresho na ujenzi wa majengo ya kisasa yanayofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Mhe. Faidha aliagiza kulindwa kwa maeneo yote ya umma na kusisitiza kuwa, endapo kuna watu wengine binafsi wanaovamia maeneo ya Serikali, yakiwemo hifadhi za barabara, kuondoka mapema kabla ya kuanza kuleta usumbufu mwingine na badala yake watafutiwe maeneo mengine ambayo yako kimkakati kwa shughuli za uzalishaji kwa wananchi.

Naye Bw. Kanyairita ambaye aliongozana na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Busega, Mhe. Christian Rugumila, alimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kumaliza mgogoro huo.

“Tunakupongeza Mkuu wa Wilaya kwa hatua hii uliochukua, kwani sote tunahudumia Wananchi wa Wilaya ya Busega. Pia tunashukuru kwa kutambua umuhimu wa huduma za kimahakama zinazotolewa katika eneo hili,” alisema Kanyairita.

Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Faidha Suleiman (katikati) akizungumza jambo na Mtendaji wa Mahakama Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita.

Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Faidha Suleiman (katikati) akizungumza na Viongozi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Halmashauri  Mahakama kuhusiana na namna ya kutatua mgogoro uliopo.

Mtendaji wa Mahakama Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita akionyesha mipaka ya eneo la Mahakama ya Mwanzo Nyashimo.

Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Faidha Suleiman (kushoto) akizungumza na Viongozi mbalimbali baada maridhiano.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Musoma)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni