Jumanne, 4 Juni 2024

NEEMA YAFUNGULIWA SINGIDA

  • Wananchi maelfu kunufaika ujenzi wa kituo jumuishi. 

 

Na FAUSTINE KAPAMA - Mahakama, Singida. 

 

Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Singida unatarajia kunufaisha maelfu ya Wananchi Mkoani hapa wakati wa utekelezaji wa mradi huo ambao umeshaanza tangu Mei 9, 2024. 

 

Akizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerard Chami katika eneo la mradi jana tarehe 3 Juni, 2024, Mhandisi Charles Njowero alisema kuwa wameamua kuwekeza nguvu kubwa ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati. 

 

"Tutakuwa na watalaam waajiriwa zaidi ya sita wakiwemo; Meneja Mradi, Mhandisi wa Mradi, Mtalaam wa Afya na Usalama mahala pa kazi, Mazingira, Mkadiliaji Majenzi  na wengine. Lengo ni kuhakikisha kazi ya ujenzi inafanyika kwa viwango vinavyotakiwa kama mkataba unavyoeleza," alisema. 

 

Mhandisi Njowero alieleza pia kuwa wakati wa utekelezaji wa mradi huo wanatarajia kuajiri vibarua zaidi ya 500 na mradi utanufaisha maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Singida, wakiwemo Wafanyabiasha, Bodaboda, Mama Lishe na wengine wengi. 

 

"Uchumi utapanda mara dufu kwa Mwananchi mmoja mmoja hapa Singida. Wafanyabiashara mbalimbali kama wa vifaa vya ujenzi kama simenti, mbao, misumali, bati, viatu na wengine watanufaika sana. Bodaboda kwa ajili ya usafiri wa kukimbia hapa na pale na mama lishe kwa ajili ya chakula ndiyo usiseme. Mradi huu ni neema Singida, " alisema. 

 

Naye Mtendaji wa Mahakama Singida, Bw. Yusuf Kasuka, alisema kwa sasa Mkandarasi anaendelea na shughuli za awali za ujenzi, ikiwemo kusafisha eneo la ujenzi wa mradi na kubomoa jengo la zamani (chakavu). Kituo hicho kinajengwa katika eneo ilipokuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mtaa wa Bomani katika Manispaa ya Singida.

 

"Tunasubiri kibali cha mazingira kubomoa jengo hili kutokana na mabati ya asbesto yaliyotumika kuliezeka. Watu wa mazingira wanataratibu zao namna ya kuyaezua. Tunafuatilia kwa karibu kila kitu kinachoendelea kuhakikisha Mkandarasi anatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba," alisema. 

 

Ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi Singida lenye mapana na marefu ya mita 58 kwa 37 na kwenda juu kwa ghorofa nne, unatarajiwa kugharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 10 za Kitanzania kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupita Kitengo cha Maboresho ya Mahakama (JDU) cha Mahakama ya Tanzania.


Mwonekano wa jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida  kwa nje kinapojengwa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Singida (picha mbili juu na chini).





Mwonekano wa jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida  kwa ndani kinapojengwa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Singida (picha tatu juu na chini).




Mtendaji wa Mahakama Singida, Bw. Yusuf Kasuka (katikati) akimwelezea Mkuu wa Kitengo cha ElimuHabari na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerard Chami (kushoto) namna mradi huo utakavyotekelezwa. Kulia ni Mhandisi Charles Njowero.


Kazi ya kusafisha eneo la mradi inaendelea (juu na chini).

 

Eneo la kuingilia katika eneo la mradi (juu na chini).

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni