Jumatatu, 3 Juni 2024

WATUMISHI MAHAKAMA KANDA YA SHINYANGA WAKUMBUSHWA KUFUATILIA MITANDAO YA KIJAMII YA MAHAKAMA

Na Naumi Shekilindi, Mahakama-Simiyu

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali amewataka Watumishi wa Kanda hiyo kufuatilia taarifa mbalimbali zinazowekwa kwenye mitandao ya kijamiii ya Mahakama ili kujifunza na kujua yanayoendela ndani ya Mhimili huo katika maeneo mbalimbali.

Mhe. Mahimbali alitoa rai hiyo wakati akizungumza na Watumishi wa Mahakama za Mkoa wa Simiyu katika kikao kazi kilichofanyika tarehe 31 Mei, 2024 katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu.

“Zipo jukwaa mbalimbali za Mahakama ambazo zinatoa taarifa juu ya yanayojiri kutoka maeneo mbalimbali, ni muhimu sana kwa watumishi wote wa Mahakama kufuatilia na kujifunza kupitia mitandao hiyo, nina imani watumishi wengi mnazo simu janja ambazo zinawawezesha kufuatilia mitandao yetu ya Kijamii, hivyo niwasisitize kuhakikisha mnafuatilia mitandao hiyo ili kujielimisha na kupata taarifa mbalimbali zinazotolewa na Mahakama ya Tanzania,’’ alisema Mhe. Mahimbali.

Mhe. Mahimbali aliwasisitiza Watumishi hao, kufuatilia taarifa zinazotolewa na Mahakama kutoka maeneo mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii ili kujifunza na kufahamu yanayoendelea kutoka Mahakama zingine sambamba na kujionea maboresho yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania kote nchini.

Hali kadhalika, Jaji Mfawidhi huyo, alitoa rai kwa watumishi wote wa Mahakama kujenga mazoea ya kujisomea kupitia ‘forum’ hizo pamoja na maeneo mengine, ambapo alisisitiza, “tujenge mazoea ya kujisomea na kutafuta maarifa katika maeneo mbalimbali tofauti na fani mlizosomea, kuongeza maarifa katika uchumi, sosholojia na maeneo mengine.”

Naye, Mwakilishi wa Kitengo cha Habari, Mahakama Kanda ya Shinyanga, Bw. Emmanuel Oguda alitoa ufafanuzi na kuelezea manufaa yatokanayo na mitandao ya Mahakama ikiwa ni pamoja na kupata maagizo yatolewayo na Viongozi Wakuu wa Mahakama.

Bw. Oguda aliwakumbusha watumishi hao kufuatilia mitandao hiyo ambayo ni pamoja na Tovuti ‘Website’ ya Mahakama ya www.judiciary.go.tz, Blogu ya tanzaniajudiciary.blogspot.com, Instagram (judiciarytanzania), Facebook (Mahakama ya Tanzania), Youtube (Mahakama ya Tanzania) na ‘Twitter-X’ (judiciarytz). 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali akizungumza na Mahakimu pamoja na Watumishi wengine wa Mahakama ya Mkoa wa Simiyu wakati wa kikao kazi na watumishi hao uliofanyika tarehe 31 Mei, 2024.

 
Sehemu ya Mahakimu na Watumishi wengine wa Mahakama Mkoa wa Simiyu wakiwa katika kikao kazi cha Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali (hayupo katika picha).

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Asha Mwetindwa akizungumza na Watumishi wa Mkoa wa Simiyu wakati wa kikao cha Jaji Mfawidhi na Watumishi hao kilichofanyika hivi karibuni.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mhe. Martha Mahumbuga akisikiliza kwa makini kinachojiri katika kikao kazi hicho.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Bariadi, Mhe. Caroline Kiliwa (kushoto), Afisa Tawala wa Mahakama ya hakimu Mkazi Simiyu, Bi. Naumi Shekilindi (kulia) pamoja na sehemu ya  Watumishi wa Mahakama Simiyu wakifuatilia kwa makini kilichokuwa kikiendelea katika kikao kazi cha Jaji Mfawidhi Kanda ya Shinyanga.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni