Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Arusha
Mkuu wa wilaya ya Arumeru na Mwenyekiti wa Kamati ya
Maadili ya Maafisa Mahakama wilayani humo, Mhandisi Emmanuela Kaganda amesisitiza
umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano kati ya Mihimili ya Dola ili kuwezesha
wananchi kupata haki kwa wakati.
Akizungumza wakati wa Utoaji wa Elimu kwa wajumbe wa
Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya Wilaya hiyo jana tarehe 8 Julai, 2024,
Mkuu huyo wa wilaya alisema ushirikiano kati ya Mahakama na Serikali ni muhimu
kwa kuwa Mihimili yote inalenga kumstawisha Mwananchi wa Tanzania.
“Natambua umuhimu wa Mahakama na ushirikiano unaohitajika
kwani bila ushirikiano kati ya mihimili ya Dola, Mwananchi hatapata haki kwa
wakati”, alisema.
Aidha, Mhandisi Kaganda ameihakikishia Tume ya Utumishi
wa Mahakama kuwa Kamati anayoiongoza itafanya vikao vyake vilivyopangwa kwa
mujibu wa Sheria. Vikao hivyo hutakiwa kufanyika mara nne kwa mwaka.
Akizungumzia utekelezaji wa majukumu ya Kamati, Mkuu huyo
wa wilaya alisema Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Wilaya ya Arumeru
itatekeleza vema jukumu lake la kusimamia Maadili ya Mahakimu kwa kufuata
kanuni, mwongozo na taratibu zilizowekwa ili kutenda haki.
Mkuu huyo wa Wilaya pia aliwashukuru Watumishi wa
Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuona umuhimu wa kufika
wilayani Arumeru na kutoa elimu kuhusu uendeshaji wa Kamati za Maadili ya
Maafisa Mahakama kwa wajumbe wa Kamati hiyo.
Kwa
upande wake, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu)
Bi. Alesia Alex Mbuya alisisitiza
umuhimu wa wajumbe wa Kamati kula viapo kabla ya kuanza kushughulikia mashauri
ya kinidhamu na kukabidhiana nyaraka muhimu zinazotumika katika kutekeleza kazi
za Kamati za Maadili pale inapotokea uhamisho ili kuwe na muendelezo wa
utekelezaji wa majukumu ya Kamati hizo.
Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya
inaundwa na wajumbe wafuatao; Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati,
Katibu Tawala wa wilaya (Katibu), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya,
wajumbe wawili walioteuliwa na Mkuu wa Wilaya na Maafisa Mahakama wawili
wanaoteuliwa na Jaji Mfawidhi.
Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya
watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia
kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama
Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake
kwenye Kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati
za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo
cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya
Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili
kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la
kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja
na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa
Mahakama Sura ya 237.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni