- Awataka Mahakimu Wafawidhi kusimamia kikamilifu uendeshaji wa mashauri
- Abainisha mafanikio lukuki yaliyofikiwa ndani ya miezi sita
- Mahakama Pwani, Rufiji vinara uondoshaji wa mashauri
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Mussa Maghimbi leo tarehe 10 Julai, 2024 ameongoza Kikao cha Kamati ya Uongozi kufanya tathmini na kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji kwa kipindi cha Januari hadi Juni, 2024.
Akizungumza wakati anafungua kikao hicho, Mhe. Maghimbi amewataka Viongozi wote kwenda pamoja wanapotekeleza majukumu yao ili kufikia malengo ya Taasisi katika muktadha mzima wa utoaji haki kwa wananchi.
Amebainisha mafanikio kadhaa ambayo yamefikiwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo usikilizaji wa mashauri katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni, 2024.
Jaji Mfawidhi amewaeleza wajumbe wa kikao kuwa Kanda yake ilivuka mwaka 2024 na mashauri 8,146, mashauri yaliyofunguliwa Janunari hadi Juni, 2024 yalikuwa 12,056, hivyo kufanya jumla ya mashauri yote 20,202.
“Mashauri yaliyoisha kati ya Januari na Juni, 2024 ni 10,697 na mashauri 9,646 yalibaki. Kiwango cha uondoshaji wa mashauri kilikuwa asilimia 89 na umalizaji wa mashauri ulikuwa asilimia 53,” amesema.
Kufuatia takwimu hizo, Mhe. Maghimbi amewataka Mahakimu Wafawidhi katika ngazi zote kusimamia kikamilifu uendeshaji wa mashauri katika maeneo yao ili kuongeza kasi ya uondoshaji na umalizaji.
“Pamoja na mafanikio haya, mimi siridhishwi na utendaji kazi kwa ujumla. Lazima tutafute namna ya kutoka hapa tulipo. Ngoja niwaambie kitu, hakuna ndugu yako kazini, tusichekeane. Tusipende kupendwa na wale tunaowaongoza, kila mtu afanye kazi na kutekeleza majukumu aliyopangiwa,” amesema.
Jaji Mfawidhi aliwanyoshea vidole watumishi na Viongozi wanaong’ang’ani kutumia makaratasi kwenye shughuli za kimahakama na kuchelewa kuhuisha mashauri kwenye mfumo.
“Sasa mahakamani kilichotawala ni teknolojia. Nyinyi Watendaji, tutaulizana maswali kama nikiwaona mnanunua karatasi kwa ajili sijui ya kuandaa mienendo au sijui kitu gani,” Mhe. Maghimbi amesema.
Hata hivyo, Jaji Mfawidhi ameipongeza Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani kwa kuwa kinara kwenye uondoshaji wa mashauri baada ya kufikisha asilimia 118, huku Mahakama ya Wilaya Rufiji nayo ikipaa kwa asilimia 175 kwa upande wa Mahakama za Wilaya katika Kanda hiyo.
Mhe. Maghimbi amebainisha pia kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Rufiji imefanya vizuri kwenye umalizaji wa mashauri kwa asilimia 92, huku Mahakama za Wilaya Mkuranga na Mafia zikichuana kileleni kwa asilimia 71.
Kadhalika, Jaji Mfawidhi amebainisha kuwa jumla ya mashauri 40 yalipangwa katika kipindi husika ambapo 36 yalimalizika yakiwemo manne ya ugaidi, manne ya dawa za kulevya na 28 ya madai.
Naye Mtendaji wa Mahakama, Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka, akiwasilisha taarifa ya utendaji kwenye kikao hicho, ameeleza kuwa Mahakama katika Kanda hiyo imeendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama nguzo ya pili kwa kupokea, kusikiliza na kutolea uamuzi mashauri mbalimbali kwa mujibu wa sheria.
“Umalizaji wa mashauri kwa wakati umekuwa ukifanyika kwa ufanisi na weledi wa kutosha na kupelekea kupunguza malalamiko ya wananchi ya kucheleweshwa kwa mashauri,” amesema.
Aidha, Mtendaji ameeleza pia kuwa mashauri yamekuwa yakisajiliwa kwenye mfumo wa e-CMS na kuhuishwa kwa wakati, hali iliyowezesha taarifa hizo kupatikana kwa urahisi katika mfumo huo, japokuwa baadhi ya Mahakama bado hazifanyi vizuri katika eneo hilo.
Bw. Mashaka amebainisha kuwa kumekuwa na ongezeko la usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao na kwamba jitihada kubwa zinafanyika kuhakikisha mashauri yanayosajiliwa mahakamani yanafanyiwa kazi kwa kuzingatia miongozo iliyopo na viwango vilivyowekwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni