Jumamosi, 20 Julai 2024

JAJI MKUU ZANZIBAR AHITIMISHA KIKAO KAZI KUJADILI UTOAJI HAKI KAZI TANZANIA

  • Atamani mabadiliko ya sheria yanayokwenda na wakati, mazingira halisi ya Tanzania

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Zanzibar

Kikao Kazi baina ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Viongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, kilichokuwa kinafanyika Visiwani hapa kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kuboresha sheria na utoaji haki kazi Tanzania kimehitimishwa leo tarehe 20 Julai, 2024.

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla ndiye aliyekuwa mhenio rasmi katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Viongozi wengine wa Mahakama, wakiwemo Viongozi wa Mahakama ya Tanzania na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

Akizungumza katikla hafla hiyo, Mhe. Abdalla amesema kuwa Kikao Kazi hicho kimekuwa shirikishi kwa Majaji wa Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na maafisa wengine wakuu na wadau mbalimbali wa masuala ya kazi wa Tanzania.

Amesema kuwa Kikao Kazi hicho kitasaidia kukuza na kudumisha muungano wa Tanzania na kujenga uwelewa na tafsiri ya pamoja katika vifungu mbalimbali vya sheria za kazi na kukuza falsafa ya sheria (jurisprudence) kwenye utatuzi wa migogoro ya kazi na kuleta tija na ufanisi kwa Taifa.

“Ninaamini kwa udhati kuwa, utekelezaji wa maazimio yatokanayo na kikao hiki utakuwa ni chachu ya mabadiliko ya sheria zetu za kazi zitakazokwenda sambamba na wakati pamoja mazingira halisi ya nchi yetu na mikataba mbalimbali ya kimataifa na hivyo kukidhi matarajio ya Serikali zetu na wafanyakazi wote kwa ujumla,” Jaji Mkuu wa Zanzibar amesema.

Amebainisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa mstari wa mbele katika kuziimarisha na kuzijengea uwezo Mahakama pamoja na vyombo vyote vya utatuzi wa migogoro ya kazi, ikiwa ni pamoja na kuwa na sheria rafiki za kazi zinazoakisi mazingira halisi ya nchi.

Hivyo, Mhe. Abdalla akasema Watendaji wa Mahakama na wadau wote wa Taasisi za Kazi hawana budi kutumia umahiri na uweledi katika kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanapata nafuu na viliwazo vinavyostahiki, ikiwa ni pamoja na kupata fidia za haraka kutokana na majanga mbalimbali yanayowapata kama vile vifo, maradhi, ulemavu wakiwa kwenye mchakato wa kutekeleza majukumu yao. 

“Ni lazima tuwe na mifumo inayosomana kwa lengo la kuondoa urasimu na pingamizi zote zinazochelewesha fidia kwa wafanyakazi. Zaidi ya hayo, ni lazima tuendelee kuwajengea uwezo watumishi wetu wa taasisi za kazi ili waweze kutoa huduma bora kwa wafanyakazi na wananchi kwa ujumla,” Jaji Mkuu wa Zanzibar amesema.

Kabla ya kuhitimisha kikao kazi hicho, washiriki walipitishwa kwenye mada mbili. Mada ya kwanza ilihusu Taasisi ya Sheria za Kazi iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Uamuzi kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi na Mikataba ya Kimataifa kuhusiana na Usalama wa Kazi na Fidia kwa Wafanyakazi iliyowasilishwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Biswalo Mganga.

Washiriki wa Kikao Kazi hicho walikuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Masjala mbalimbali, Majaji wa Mahkama Kuu Zanzibar, Kamishna wa Kazi, Watendaji wa Mahakama Kuu Divisheni na Kanda, Naibu Wasajili na Watendaji, watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na wadau wengine wa haki kazi.

Kikao Kazi hicho kilifunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla jana tarehe 18 Julai, 2024.

 

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla akizungumza wakati anahitimisha Kikao Kazi baina ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Viongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Yose Mlyambina akiwasilisha neon la utangulizi kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu wa Zanzibar kuhitimisha Kikao Kazi hicho.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Biswalo Mganga akiwasilisha mada kutusu Mikataba ya Kimataifa kuhusiana na Usalama wa Kazi na Fidia kwa Wafanyakazi.

Mkurugenzi wa Uamuzi kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Dkt. Vallence Wambali akiwasilisha mada kuhusu Taasisi ya Sheria za Kazi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma wakati wa Kikao Kazi hicho.


Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahkama Kuu Zanzibar (juu na chini) wakiwa kwenye siku ya mwisho ya Kikao Kazi hicho.



Sehemu nyingine ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahkama Kuu Zanzibar (juu na chini) wakifuatilia yale yaliyokuwa yanajiri.


Sehemu nyingine ya tatu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahkama Kuu Zanzibar (juu na picha mbili chini) wakiwa kwenye siku ya mwisho ya Kikao Kazi hicho.



Sehemu ya nne ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahkama Kuu Zanzibar, Watendaji wa Mahakama Kuu Divisheni na Kanda, Msajili wa Mahakama Kuu na Naibu Wasajili (juu na picha mbili chini) wakiwa kwenye siku ya mwisho ya Kikao Kazi hicho.




























Hakuna maoni:

Chapisha Maoni