Jumanne, 23 Julai 2024

MAHAKAMA KANDA YA KIGOMA YAPOKEA JAJI MPYA

Ni Jaji Projestus Kahyoza

Aonesha furaha ya kupangiwa Kituo hicho

Aidan Robert, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile leo tarehe 23 Julai, 2024 amewaongoza Watumishi wa Kanda hiyo katika viwanja vya Mahakama Kuu  kumpokea Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza, Jaji wa Mahakama Kuu ambaye amepangiwa kazi katika Kituo hicho.

Akizungumza mara baada ya kumpokea Jaji Kahyoza, Mhe. Rwizile amemueleza kuwa, Mahakama Kanda ya Kigoma ina timu nzuri ya kazi na vilevile ni sehemu nzuri ya kufanya kazi kwa kuwa mazingira na hali ya hewa ni nzuri.

Kwa upande wake Mhe. Kahyoza ameushukuru uongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma ukiongozwa na Jaji Mfawidhi kwa mapokezi mazuri waliyoyafanya katika kituo chake kipya cha kazi na kuongeza kwamba, Mkoa wa Kigoma ilikuwa ni ndoto yake ya siku nyingi kufanyia kazi.  

“Wametimiza ndoto yangu ya siku nyingi ya kunipangia Kituo hiki cha Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma,” amesema Jaji Kahyoza.

Mhe. Kahyoza ni miongoni mwa Majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Ujio wa Jaji huyo utaongeza nguvu katika usikilizwaji wa mashauri katika Kanda hiyo, hata hivyo Kanda hiyo itakuwa na jumla ya Majaji watatu ambao wamejipanga kuhakikisha mashauri yanayosajiliwa yanasikilizwa na kuamuliwa kwa haraka ili kuendana Dira ya Mahakama ya utoaji wa haki sawa kwa wote na kwa wakati.

Jaji Mfawidhi  wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (kulia) akisalimiana na kumkaribisha Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma mara baada ya kuwasili leo tarehe 23 Julai, 2024 kwa lengo la kuripoti katika Kituo chake kipya cha kazi.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza (kushoto) akipokea zawadi ya ua kama alama ya ukaribisho katika Kanda hiyo. Anayemkabidhi ua ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Eva Mushi.

Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma akizungumza jambo mara baada kusaini kitabu cha wageni  katika ofisi ya Jaji Mfawidhi Kanda ya Kigoma aliporipoti leo tarehe 23 Julai, 2024. 

Jaji Mfawidhi  wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (kulia) akisikiliza kwa makini jambo alilokuwa akizungumza Mhe. Kahyoza (katikati). Kushoto ni Jaji wa Kanda hiyo, Mhe. John Francis Nkwabi akifuatilia mazungumzo katika ofisi ya Jaji Mfawidhi Mahakama Kanda ya Kigoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma mara baada ya kumpokea Jaji mpya wa Mahakama Kuu, Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza (wa pili kulia) aliyepangiwa kufanya kazi katika Kituo hicho. Wa pili kushoto Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe.  John Francis Nkwabi, wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay na wa kwanza kushoto ni  Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni