Alhamisi, 4 Julai 2024

MTENDAJI MKUU ATETA NA WAANDISHI WA HABARI

  • Abainisha maendeleo ya uboreshaji huduma mahakamani kabla na baada ya uhuru

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa kuboresha huduma za utoaji haki nchini kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo ongezeko la Majaji na Mahakimu, uimarishaji wa miundombinu na maendeleo katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Hayo yamebainishwa leo tarehe 4 Julai, 2024 na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alipokuwa anaongea na Waandishi wa Habari kuhusu historia na muundo wa Mahakama kabla na baada ya uhuru.

Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia eneo la watumishi, Prof. Ole Gabriel amebainisha kuwa katika kipindi cha ukoloni, Majaji waliokuwa wanahudumu Mahakama Kuu walikuwa wawili, ukilinganisha na sasa baada ya uhuru ambapo ongezeko limekuwa kubwa na kufikia Majaji 109.

“Wakati wa uhuru, Mahakama Kuu ilikuwa na masjala mbili za (Dar es Salaam na Arusha na Majaji walikuwa saba. Hadi sasa, idadi ya Majaji wa Mahakama Kuu imeongezeka na kufikia 109 na Masjala za Mahakama Kuu zimeongezeka kutoka mbili hadi kufikia 19,” amesema.

Mtendaji Mkuu amebainisha pia kuwa Mahakama ya Rufani ilianza mwaka 1979 na Majaji watano, akiwemo Jaji Mkuu waliokuwa wakifanya kazi katika Masjala za Dar es Salaam na Zanzibar. 

“Hadi sasa mwaka huu wa 2024, Mahakama ya Rufani ina Majaji 35, kulinganisha na Majaji watano mwaka 1979, ongezeko hilo likiwa sawa na asilimia 600,” amesema.

Kadhalika, Prof. Ole Gabriel ameeleza kuwa idadi ya Watumishi katika kada mbalimbali imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo kwa sasa wamefikia 5,850, kulinganisha na idadi ndogo kabla ya uhuru. 

Akizungumzia miundombinu, Mtendaji Mkuu amesema, “Majengo ya Mahakama katika kipindi cha nyuma yalikuwa duni na sasa yameboreshwa.”

Prof. Ole Gabriel amesema kumekuwepo pia na ongezeko la idadi ya Mahakama katika ngazi zote ambapo kwa sasa huduma ya Mahakama Kuu inapatikana katika Kanda 19, Divisheni nne za Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi 30, Mahakama za Wilaya 135 na Mahakama za Mwanzo 960.

“Tumeanzisha pia dhana ya mfumo Jumuishi ya Utoaji Haki (IJC). Vituo sita vya Temeke, Kinondoni, Mwanza, Dodoma, Arusha na Morogoro vinafanya kazi kwa sasa na vingine tisa vinajengwa, ikiwepo katika Visiwa vya Pemba,” amesema.

Akizungumzia maendeleo katika TEHAMA, Mtendaji Mkuu amebainisha kuwa tokea enzi ya Ukoloni mienendo ya kumbukumbu za Mahakama katika ngazi zote imekuwa ikichukuliwa mahakamani kwa mkono. 

Amesema kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha ucheleweshaji wa utoaji haki. Hata hivyo, Prof. Ole Gabriel amebainisha kuwa Mahakama kwa sasa imeanza kutumia mifumo ya teknolojia ya kisasa.

“Kwa sasa Mahakama ya Tanzania inatumia mifumo 17 ya TEHAMA katika kuendesha shughuli zake na kuifanya kuwa ya kwanza miongoni mwa Taasisi za umma hapa nchini,” amesema.

Ametaja baadhi ya mifumo hiyo ni mfumo wa kurekodi mwenendo wa mashauri mahakamani, usajili wa mashauri na kuhuisha katika mfumo wa usimamizi wa mashauri, maktaba mtandao ya kisasa (e-library), matumizi ya tovuti, ofisi mtandao na upokeaji wa mrejesho kutoka kwa wananchi.

Mahakama ya Tanzania imeanzisha utaratibu wa kuzungumza na Waandishi wa Habari kila mwanzo wa mwezi ili kutoa taarifa ya masuala mbalimbali yanayoendelea ndani ya Mhimili huo lengo likiwa kuwahabarisha wananchi kuhusu maendeleo ya huduma ya utoaji wa haki nchini.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa anaongea na Waandishi wa Habari leo tarehe 4 Julai, 2024.


Sehemu ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo katika picha).

Baadhi ya Watendaji na Naibu Msajili waliohudhuria mkutano kati ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Waandishi wa Habari uliofanyika leo tarehe 04 Julai, 2024 kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mtendaji wa Mahakama Kuu-Divisheni, Bi. Mary Shirima, kushoto ni Mtendaji wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Bw. Samson Mashalla na kulia ni Naibu Msajili wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Evodia Kyaruzi.
Sehemu ya Watumishi na Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo katika picha). Walioketi upande wa kwanza wa kushoto mbele ni Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Gerard Julius Chami, nyuma yake ni Katibu wa Mtendaji Mkuu, Bw. Majuto Mdenya.
 Waandishi wa Habari pamoja na baadhi wa watumishi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo katika picha).


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni