Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Kiteto Manyara
Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na
Nidhamu) Bi. Alesia Alex Mbuya ametoa wito kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya
Maafisa Mahakama kufanya vikao vya Kamati hizo kwa kuwa vikao hivyo viko kwa
mujibu wa Sheria.
Akizungumza
na Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Wilaya ya Kiteto leo tarehe
4 Julai, 2024 mjini Kibaya, Naibu Katibu alisema Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya
Usimamizi wa Mahakama Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji
wa majukumu yake kwenye Kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo ambapo Kamati
za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya ni mojawapo.
Alisema kukutana kwa wajumbe wa Kamati mara nne kwa mwaka
kama ilivyopangwa kutasaidia Kamati kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kutoa
haki kwa wakati. Alifafanua kuwa endapo Kamati itakuwa na shauri la
kushughulikia haina budi kulikamilisha ndani ya siku 90 zilizowekwa kisheria na
endapo kutakuwa na haja ya kuongeza muda, Jaji Mfawidhi ataongeza siku
zisizozidi 30.
Aidha, Naibu Katibu Alesia pia alisisitiza umuhimu wa
wajumbe wa Kamati kula viapo kabla ya kuanza kushughulikia mashauri ya kinidhamu.
”Kwa upande wa mashahidi wa shauri, hawa wanapaswa kula
kiapo mbele ya Kamati”, alisisitiza.
Kuhusu nyaraka zinazotumika katika kutekeleza kazi za
Kamati za Maadili, Bi. Mbuya alisema ni muhimu kwa Wenyeviti wa Kamati hizo
kukabidhiana nyaraka hizo pale kunapotokea uhamisho ili kuwe na muendelezo wa
utekelezaji wa majukumu ya Kamati hizo.
Naye Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Kiteto Bw. Fadhili
Dedan Alexander alisema elimu waliyopatiwa na Tume kuhusu utekelezaji wa majukumu
ya Kamati za Maadili itawasaidia wajumbe kutekeleza majukumu yao ipasavyo na
kwa usahihi. Aliongeza kuwa ziara ya Watumishi wa Sekretarieti ya Tume ya
Utumishi wa Mahakama Wilayani Kiteto itazihuisha Kamati hizo.
Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya inaundwa
na wajumbe wafuatao; Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati, Katibu
Tawala wa wilaya (Katibu), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, wajumbe
wawili walioteuliwa na Mkuu wa Wilaya na Maafisa Mahakama wawili wanaoteuliwa
na Jaji Mfawidhi.
Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya
watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia
kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama
Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake
kwenye Kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati
za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo
cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya
Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili
kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la
kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja
na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa
Mahakama Sura ya 237.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni