Jumanne, 30 Julai 2024

TARATIBU ZA KUSHUGHULIKIA UFUNGAJI WA MASHAURI YA MIRATHI ZIFUATWE – JAJI RWIZILE

Na AIDAN ROBERT, Mahakama- Kigoma 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile ametoa rai kwa Mahakimu wa Kanda hiyo kuzingatia utaratibu wa kufunga mashauri ya mirathi mara baada ya kumteua msimamizi wa mirathi na kumpa majukumu ya kutambua na kukusanya mali za marehemu na kisha kusajili orodha ya mali hizo mahakamani ili Mahakama iendelee na utaratibu wa kusimamia ugawaji kwa warithi halali wa mali za marehemu. 

Mhe. Rwizile aliyasema hayo hivi karibuni katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma wakati akifungua mafunzo ya siku moja yaliyofanyika kwa makundi mawili ambapo kundi la kwanza liliwakutanisha Mahakimu 27 na Maafisa wa Kada mbalimbali 12.

‘‘Ufungaji wa mirathi kwa kuzingatia hatua zote na kufuatilia kwa karibu utekelezwaji wa amri za Mahakama zote utapunguza migogoro ya familia kwenye ugawaji wa mirathi yao na pia utaondoa mlundikano wa fedha katika akaunti mirathi za Mahakama,’’ alisema Jaji Rwizile.

Jaji Mfawidhi huyo alisema lengo la kuandaa mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Maafisa hao ili kuboresha huduma za Mahakama Kanda ya Kigoma kuanzia Mahakama ya Mwanzo mpaka Mahakama Kuu na kuongeza kuwa, hatua hiyo italeta hali ya kuongeza imani kwa wananchi wanaowahudumia kwa kuona kuna maboresho ya miundombinu na huduma zake maana jamii inatarajia Mahakama yenye mambo ya kisasa katika kutoa huduma zake na kufuata taratibu zote utoaji huduma kwa wateja.

Mada zilizotolewa katika mafunzo hayo ni pamoja na utaratibu wa kushughulikia mashauri ya mirathi. Aidha, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi alipata fursa ya kuwa sehemu ya watoa mada juu ya usikilizwaji wa awali mashauri ya jinai.

Mhe. Nkwabi alisisitiza juu ya kufuata hatua zote za sheria katika kusikiliza mashauri ya mauaji kwa hatua za awali.

Watoa mada wengine ni Afisa Manunuzi kutoka Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini  TARURA, Bw. Isaya Mbuba, ambaye alifundisha juu ya Matumizi ya Mfumo mpya wa Manunuzi (NeST) na Afisa Mafao kutoka Mfuko wa Hifadhi wa Jamii PSSSF, Bw. Thomas aliyewasilisha mada ya mfumo wa (PSSSF Membership Portal).

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay alisema Kanda hiyo imejipanga kuhakikisha watumishi waliopo wanakuwa na weledi katika kushughulikia mirathi na usikilizwaji wa awali wa mashauri ya Jinai na Mfumo wa Kuratibu na Kusikiliza Mashauri Mahakamani (e-CMS) pamoja na Mfumo wa Utaratibu wa kushughulikia mashauri ya mirathi.

Bw. Matotay alitoa rai kwa washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha matarajio ya Mahakama kwao yanatimia kwa kiwango kinachokubalika katika maeneo yote muhimu ambayo imeweka vipaumbele kwa kuboresha huduma katika Mahakama zote za Kanda ya Kigoma.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Kibondo, Bi. Naomi Chawe alisema mafunzo hayo yamewajengea uwezo mkubwa watumishi hao kwa kuwa maeneo yaliyofundishwa ni maeneo muhimu  katika kuboresha huduma za Mahakama pamoja na usikilizwaji wa Mashauri katika Kanda ya Kigoma.

Aliushukuru uongozi wa Kanda kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yanaongeza ufanisi wa kila Afisa katika eneo lake la huduma sambamba na kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma yalihudhuriwa na Majaji wa Kanda hiyo, Mhe. John Francis Nkwabi pamoja na Mhe. Projestus Kahyoza na Watumishi wengine wa Kanda hiyo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (aliyesimama) akisisitiza jambo wakati akifundisha mada ya utaratibu wa kushughulikia mashauri ya mirathi katika mafunzo ya siku moja kwa watumishi wa Kanda hiyo yaliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma.
Sehemu ya Mahakimu wa Kanda ya Kigoma wakifuatilia kwa ukaribu mada iliyokuwa ikitolewa na moja wa watoa mada katika mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa hao katika maeneo mbalimbali ya shughuli za Mahakama yaliyofanyika hivi karibuni.
Afisa Utumishi  wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma Bw. Festo Sanga akisisitiza jambo wakati wa kuwasilisha mada ya mfumo wa e-Utumishi (ESS) kwa washiriki wa mafunzo hayo, yaliyoandaliwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo.
Afisa Mafao kutoka Mfuko wa Hifadhi wa Jamii PSSSF, Bw. Thomas akiwasilisha mada ya Mfumo wa (PSSSF Membership Portal) kwa washiriki wa mafunzo yalioandaliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma katika kuwajengea uwezo.
Afisa Manunuzi wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Bw. Isaya Mbuba akifundisha juu ya matumizi ya Mfumo mpya wa Manunuzi (NeST) kwa Maafisa wa Mahakama ili kuwajengea uwezo Maafisa hao katika eneo la manunuzi ya Serikali kwa njia ya Mfumo.
Jaji Mfawidhi  wa Mahakama Kanda ya kigoma Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo, wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza, wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay na wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki. Waliosimama nyuma ni Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Wilaya na Mahakimu wa  Mahakama za Mwanzo Kanda ya Kigoma.
Jaji Mfawidhi  wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya washiriki wa mafunzo. Wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza, wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay na wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki. Waliosimama ni Maafisa Utumishi na Tawala kutoka Mahakama za Wilaya Kigoma.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni