Jumanne, 2 Julai 2024

UJENZI WA MAHAKAMA YA WILAYA CHAMWINO WAANZA

Na TAWANI SALUM-Mahakama, Chamwino Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel jana tarehe 1 Julai, 2024 amekabidhi kwa Mkandalsi Molad eneo itakapojengwa Mahakama ya Wilaya Chamwino.

Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Ole Gabriel aliomba ushirikiano na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili kuhakikisha ujenzi wa Mahakama hiyo unakamilika, hivyo kukamilisha ndoto ya wanakijiji wa Chamwino.

Kadhalika, Mtendaji Mkuu alimwelekeza Mshauri Elekezi, Bw. Robert Modu, ambaye ndiye mdomo wa Mahakama kusimamia utekelezaji wa mradi huo ili kazi ifanyike kwa kasi na ubora unaotakiwa kwa mujibu wa mkataba.

“Nisingependa kuona vitu tofauti vinafanyika ambavyo ni nje ya makubaliano, na wewe Mkandarasi Molad, siyo mara yako ya kwanza kufanya kazi za Mahakama. Naomba uendelee kuwa mwaminifu kwa kutekeleza mradi kwa kasi na viwango vilevile tulivyokubaliana,” alisema.

Mtendaji Mkuu alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha ili ujenzi wa Mahakama hiyo uweze kufanyika.

“Nataka mwezi March, 2025 ujenzi huu uwe umekamilika, fanya kila linalowezekana kukamilisha ujenzi huu ndani ya wakati, tuweke nguvu zetu kwa pamoja ili kuhakikisha ujenzi unafanyika vizuri,” alisema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Hakimu Mkazi, Mhe. Francis Kishenyi. alisema watashirikiana kwa karibu na mamlaka zinazohusika kuhakikisha kuwa ujenzi huo unafanyika kikamilifu kwani wanachi wanapata shida kwa kwenda Dodoma Mjini kutafuta haki. 

Naye mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya, Bw. Benjamin Cosmas alisema watasimamia kwa karibu mradi huo ili ukamilike ndani ya muda uliopangwa kwani utatoa ajira kwa wanakijiji wa Kijiji cha Chamwino wakati wa utekelezaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji, Bw. Peter Simba alimshukuru Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kwa kuanzisha mchakato wa ujenzi wa Mahakama hiyo ambayo itapunguza kero kwa wananchi wanakwenda Dodoma Mjini kutafuta haki.


Sehemu ya wananchi na wajumbe waliohudhuria makabidhiano hayo wakimsikiliza kwa makini Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Gabriel (aliyenyoosha mkono).


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyepo katikati) akiwa katika picha ya pamoja na meza kuu katika makabidhiano ya mradi wa kujenga Mahakama ya Wilaya Chamwino Ikulu. Aliyekaa kulia kwake ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Dodoma, ambaye anahudumia na Mahakama ya Wilaya Chamwino Ikulu, Mhe. Francis Kishenyi. Kushoto kwa Mtendaji Mkuu ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Chamwino Ikulu, Bw. Said Simba Kalaita.


Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Majengo Mahakama ya Tanzania, Mhandisi Moses Lwiva akieleza jambo wakati wa kumkabidhi mkandarasi eneo la ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Chamwino Ikulu.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyevaa miwani) akisikiliza neno kutoka kwa Mkandarasi wakati wa makabadhiano eneo la ujenzi.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam) 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni