- Yahamasisha Watumishi kujiunga na SACCOS
- Yataja faida lukuki za SACCOS hiyo
Na Amani Mtinangi Mahakama Kuu Tabora
Viongozi wa Bodi ya Mahakama SACCOS jana tarehe 02 Julai, 2024 walitembelea Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora na kuonana na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora wakiwemo Majaji wa Mahakama hiyo lengo likiwa ni kufanya semina na watumishi sanjari na kuhamasisha watumishi wa Kanda hiyo wasio wanachama kujiunga na SACCOS hiyo.
Akizungumza na Viongozi wa Mahakama SACCOS ofisini kwake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi aliwapongeza kwa kufika katika Kanda hiyo na kuwahimiza kuwekeza katika fursa mbalimbali za kiuchumi ili kukuza mapato ya SACCOS, kuweka mifumo rafiki ya kujiunga hasa ya kidijitali ili kuifanya iwe ya kisasa na inayoendana na mabadiliko ya kiteknolojia.
“Kwanza niwapongeze kwa kututembelea Tabora, ninawashauri mjitahidi sana kuangalia fursa za uwekezaji muwekeze huko ili kukuza mtaji wa SACCOS na muweke mifumo rafiki ya kujiunga na kwenda kidijitali ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi. Mkifanya hivyo mtaweza kuendesha Chama vizuri na kuongeza wanachama na kuwasaidia wanachama hivyo kuwa msaada kwao na Mahakama,” alisema Mhe. Dkt. Mambi.
Naye Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Jaji Dkt. Zainab Diwa Mango aliwaeleza umuhimu wa kutumia fursa na jukwaa mbalimbali za Mahakama kuhamasisha watumishi kujiunga na chama hicho chenye fursa nyingi za kukua na kujitangaza na kuwahimiza watumishi kujiunga pamoja na kuwatafutia wanachama fursa mbalimbali za kiuchumi na kimaisha.
“Jitahidini kutumia majukwaa ya Mahakama vizuri kwa kujitangaza maana hayo ndio yenye wanachama wenu na yatawajenga kujua maoni yao, lakini pia watafutieni wanachama wenu fursa za kiuchumi na kijamii kama viwanja ili kuwainua na kuwahamasisha kujiunga na SACCOS,” alisema Mhe. Dkt. Mango.
Naye, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Bw. Emmanuel John Munda, aliwahimiza Viongozi hao kufanya ziara na semina mikoani na kuwekeza katika mifuko ya uwekezaji ili kujipatia faida kwa ajili ya wanachama wake.
“Ninawashauri muangalie namna ya kufanya ziara za mikoani na kuwekeza katika masoko mbalimbali ya mitaji na hisa, uwekezaji huo utakuza kwa haraka mtaji na kuwanufaisha wanachama,” alisema Bw. Munda.
Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mwenyekiti wa Bodi ya Mahakama SACCOS, Mhe. Ferdinand Moshi Philip alisema watumishi wa Mahakama wanapaswa kujisikia fahari kujiunga SACCOS hiyo kwa sababu ina mtaji wa kutosha na huduma zinaendelea kuboreshwa ambapo kwa sasa ipo katika maandalizi ya kuingia katika uendeshaji wake kidijitali na kwamba tayari imeanza kuwekeza katika Taasisi mbalimbali.
“Ninawasihi sana watumishi wenzangu jiungeni na mjisikie fahari kuwa wanachama wa Mahakama SACCOS kwa sababu ina mtaji wa kutosha, huduma bora na ipo mbioni kufanya shughuli zake kidijitali,” alisema Mhe. Phillip.
Ziara hiyo imeleta matunda makubwa kwa watumishi kwa kuwawezesha kuijua vizuri na kupata wanachama wapya waliojiunga ikiwemo Viongozi kadhaa wa ngazi ya juu wa Taasisi ambao walielezwa kuwa Chama hicho kimepiga hatua kubwa kuingia katika zama za kidijitali hivyo kuwa msaada kwa watumishi.
Viongozi wengine wa Mahakama waliokuwa kwenye ziara hizo ni Yusuph Kaungu Mjumbe wa Bodi na Bi. Janeth Primus Mwanisawa Mjumbe wa Bodi.
Mahakama SACCOS ni Chama kilichoundwa kwa lengo la kuwa suluhisho la mtaji, kuleta watumishi wa Mahakama pamoja ili kufanikisha malengo yao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni