Ijumaa, 19 Julai 2024

‘USHIRIKISHAJI WADAU MUHIMU KATIKA KUJENGA MAHUSIANO MAZURI, UKARIBU KWA JAMII’

  • Serikali yaonesha dhamira kuboresha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla leo tarehe 18 Julai, 2024 amefungua Kikao Kazi baina ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Viongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, ambacho kimeandaliwa kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kuboresha sheria na utoaji haki kazi Tanzania.

Ufunguzi wa Kikao Kazi hicho umehudhuriwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bi. Mary Ngeleja Maganga, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma na wengine wengi.

Washiriki wengine wa Kikao Kazi hicho ni Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Masjala mbalimbali, Majaji wa Mahkama Kuu Zanzibar, Kamishna wa Kazi, Watendaji wa Mahakama Kuu Divisheni na Kanda, Naibu Wasajili na Watendaji, watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na wadau wengine wa haki kazi.

Wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi hicho, Makamu wa Pili wa Rais alishuhudia utiaji saini wa Mkataba wa Mashirikiano kati ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kwenye maeneo yote yanayohusu ulipaji wa fidia kwa wafanyakazi.

 Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Abdulla amewataka watumishi wa Mahakama kujenga imani na uaminifu mbele ya umma kwa kutoa haki kwa watu wote na kwa wakati. Amesema kuwa ushirikishwaji wa wadau unatoa mchango mkubwa katika kujenga mahusiano mazuri na ukaribu kwa jamii.

“Kama tunavyojua kuwa Majaji na Watendaji wengine wa Mahakama tunahitajika kusikiliza mahitaji, maoni na maslahi ya wale ambao tunawahudumia. Imani yangu kuwa kwa kufanya hivyo Mahakama inaweza kujenga imani na uelewa wa pamoja juu ya namna inavyofanya kazi na wadau wake, ikiwemo WCF na ZSSF,” amesema.

Makamu wa Pili wa Rais ametumia fursa hiyo kuipongeza WCF kwa kushirikiana na ZSSF na kutekeleza kwa vitendo azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anazitaka Taasisi za umma kutekeleza majukumu yao kwa kushirikiana hapa nchini.

Ametoa wito kwa Taasisi nyingine kuiga mfano huo ambao unachangia kujenga mahusiano mema na kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku. Kadhalika, amesisitiza umuhimu wa kuunganisha mifumo yote inayohusiana na mnyororo wa utoaji haki kwa wafanyakazi ili iweze kusomana kwa kushirikiana na kupata taarifa muhimu zitakazosaidia kurahisisha utoaji wa huduma kwa wanufaika.

“Ni wazi kuwa mifumo inayosomana na kushirikiana itasaidia kupunguza makosa mbalimbali, ikiwemo kucheleweshwa haki ya mnufaika na kumpunguzia usumbufu katika kukamilisha taratibu za kupata fidia,” Mhe. Abdulla amesema.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), amesema Wizara yake pamoja na Taasisi inazozisimamia itaendelea kuimarisha ushirikiano katika pande mbili za muungano ili kuweza kuwahudumia Watanzania kwa ufanisi zaidi.

Bi Maganga amesema kuwa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi ni nguzo muhimu katika masuala ya hifadhi ya jamii kwani inalengo la kulinda nguvu kazi ya Taifa na kuwakinga na umaskini Wafanyakazi wanaopata ulemavu wakati wakitekeleza majukumu yao ya kikazi.

Amesema kuwa Sheria hiyo ni muhimu ikitekelezwa kwa haki ili kuleta tija kwa wanufanika. Katibu Mkuu amebainisha kuwa wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linapitisha Sheria hiyo liliona umuhimu wa kuweka utaratibu wa rufaa hadi ngazi ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ili kuhakikisha haki inatendeka kwa mujibu wa sheria.

“Kwa msingi huu, ni muhimu kwa Majaji pamoja na Watumishi wa WCF kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu Sheria hii. Kukosekana kwa uelewa wa pamoja kunaweza kupelekea kufanyika maamuzi yanayoweza kupoteza haki za wanufaika au kuathiri uhai na uendelevu wa mfuko…

“Vikao Kazi hivi vinatoa fursa ya kupokea maoni ya maboresho ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi kwa lengo la kuleta ufanisi wa utekelezaji wake. Katika vikao vya awali, tulipokea maoni mbalimbali ya maboresho ya Sheria hii kutoka kwa Majaji. Napenda kuwafahamisha kuwa tumeanza kufanyia kazi maoni hayo, ikiwa pamoja na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria bungeni ambao ulisomwa kwa mara ya kwanza Februari 2024,” amesema.

Bi. Maganga amebainisha pia kuwa ameunda kamati ya kuangalia utaratibu bora wa kushughulikia rufaa zinaz'otokana na maamuzi yanayofanywa na WCF kama wadau walivyoshauri hapo awali.

Katika Kikao Kazi hicho cha siku mbili, washiriki watapitishwa na kujadili mada mbalimbali, ikiwemo Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Sura No. 263, Taratibu za Madai, Tathmini za Madai ya Fidia, Taasisi ya Sheria za Kazi na Mikataba ya Kimataifa kuhusiana na Usalama wa Kazi na Fidia kwa Wafanyakazi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza leo tarehe 18 Julai, 2024 wakati anafungua Kikao Kazi baina ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Viongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi.

Viongozi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) (kulia) na Mfuko wa Hifadhi za Jamii Zanzibar (ZSSF) watia sahihi kwenye Mkataba wa Mashirikiano. Picha chini Viongozi hao wakibadilishana nyaraka za Mkataba huo.


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bi. Mary Ngeleja Maganga akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa Kikao Kazi hicho.

Meza Kuu inayoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (katikati). Wengine ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (wa tatu kusho), Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bi. Mary Ngeleja Maganga (wa tatu kulia), Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma( wa pili kulia), Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Bw. Nassor Shaban Ameir.

Meza Kuu inayoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu ya Zanzibar. Picha  chini ni Majaji kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu Zanzibar.


Meza Kuu inayoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu nyingine ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahkama Kuu Zanzibar (juu na chini).


Meza Kuu inayoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Meza Kuu inayoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda na Divisheni.

Meza Kuu inayoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa masuala ya haki kazi.

Meza Kuu inayoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa WCF na ZSSF. Picha chini ni watumishi kutoka katika mifuko hiyo.


Picha na Mwanaidi Msekwa-Mahakama, Divisheni ya Kazi

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni