Jumatatu, 22 Julai 2024

WAWAKILISHI BENKI YA DUNIA KUKAGUA MRADI WA MABORESHO WA MAHAKAMA TANZANIA

Na TAWANI SALUM – Mahakama, Dar es Salaam

Ujumbe kutoka Benki ya Dunia (WB) leo tarehe 22 Julai, 2024 umeanza ziara ya kufanya tathmini ya maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Huduma za Mahakama unaofadhiliwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki hiyo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kati ya Ujumbe huo na Mahakama ya Tanzania katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke jijini Dar es Salaam, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha amesema kuwa wawakilishi wa Benki ya Dunia wanafuatilia utekelezaji wa mradi huo ambao Benki ya Dunia inatoa fedha kupitia Serikali ya Tanzania.

“Benki ya Dunia wana utaalam mkubwa sana kwenye masuala haya kwasababu wenzetu wanafurahia uwepo wao Dunia nzima na  kila pembe,  hivyo kuja kwao hapa  na kushirikiana nao wanatuletea uzoefu na  utaalam wa kutoka  kila pembe  ya Dunia nzima,” amesema.

Mhe. Dkt. Rumisha amebainisha kuwa kwenye mradi kuna maeneo manne ambayo wamekuwa wakiyatazama, kama kuongeza uwazi na uwajibikaji, kuongeza imani ya wananchi kwa Mahakama yao na kuongeza ufikishwaji wa huduma kwa wananchi.

Kadhalika, amesema kuwa huo mradi umekuwa ukiendelea kwa muda kidogo na mwisho unakaribia kufika tarehe 30 Juni, 2025. “Tunafurahia kuona mradi unafika mwisho tukiwa tumefanikiwa katika maeneo yote tuliyokuwa tumekubaliana na wenzetu wa Benki ya Dunia,” amesema.

Jaji Rumisha amebainisha pia kuwa kwa sasa wanamalizia ujenzi wa Vituo Jumuishi tisa kwenye Mikoa mbalimbali nchini, hivyo kufikia Juni, 2025, Mikoa yote ya Tanzania itakuwa na huduma za Mahakama Kuu na watakuwa wamefikia asilimia 100 ufikiwaji wa huduma za Mahakama Kuu kwa Mikoa yote ya Tanzania.

Amesema kuwa vile vile kuna Mahakama za Mwanzo 60 zinajengwa kwa wakati mmoja ambazo nazo zitakamilika ifikapo mwezi Januari, 2025.

“Tunajivunia kuona mambo yote tuliyokubaliana na Benki ya Dunia, hadi kipimo na maeneo yote ya upimaji tumefanikiwa na kupitiliza malengo ambayo tumejiwekea,” amesema.

Kwa upande wake, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya amesema kuwa ujio huo wa wawakilishi wa Benki ya Dunia umesaidia kuiwezesha Mahakama katika utendaji wake wa kazi kwa kutumia TEHAMA katika mifumo mbalimbali, hivyo kusaidia zoezi zima la utoaji haki kwa wananchi kuwa rahisi kuliko hapo awali.

Amesisitiza kuwa watajitajitahidi kuhakikisha kuwa huo mradi unamalizika kwa kiwango cha juu ili kuweza kukidhi dhima na dira ya Mahakama ya Tanzania. Msajili Mkuu amewaomba wananchi waendelee kuiamini Mahakama kwa sababu wanaendelea kuboresha huduma ili waweze kupata haki kwa usawa na wakati.

Naye, Kiongozi Mwenza wa Ujumbe wa Benki ya Dunia, ambaye pia ni Afisa Mwandamizi kutoka Benki hiyo, Bw. Benjamin Mtesigwa, amesema kuwa wapo Tanzania kwa ajili ya tathmini ya utekelezaji wa mradi huo ambao umekuwa unatekelezwa takribani miaka minane sasa.

“Lengo la mradi huu ni kuhakikisha tunafanya maboresho katka upatikanaji wa huduma bora za kimahakama kwa wananchi wa Tanzania, huu ni utaratibu wa kawaida kabisa kati ya Benki ya Dunia na Serikali ambapo tunapata fulsa kama wataalam kuja pamoja na kujadili namna bora ya kuzidi kufanya utekelezaji wa mradi huu,” amesema.

Amebainisha kuwa taarifa walizonazo ni kwamba hawana shaka mradi huo umekuwa unatekelezwa vizuri na wanaipongeza Mahakama na uongozi wake na Serikali kwa ujumla wake kwa utekelezaji bora wa mradi huo.

“Tunajua kuna mambo mazuri yamefanyika katika vituo vya ujenzi wa Mahakama katika uboreshaji wa mifumo ya technolojia, katika mafunzo kwa Watendaji wa Mahakama na mambo mengine na kwasababu tunaingia katika mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa mradi huu, tunataka kutumia mjadala huu kuona kwa namna gani bora tunamaliza kwa kishindo zaidi.,” Bw. Mtasigwa amesema

Katika ziara yao ya wiki moja miongoni mwa wawakilishi wa ujumbe wa Benki ya Dunia waliokuja kufanya tahmini ya maboresho ya mradi huo ni Bi. Christine Owuor, Benjamin Mtesigwa, Edina Kashangaki, Roselyn Kaihula pamoja na Donna Andrews.




Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akizungumza wakati wa kikao kati ya Ujumbe wa Benki ya Dunia na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania.


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya akizungumza kwenye kikao hicho.


Kiongozi Mwenza wa Ujumbe wa Benki ya Dunia, ambaye pia ni Afisa Mwandamizi kutoka Benki hiyo, Bw. Benjamin Mtesigwa akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari baada ya kikao hicho.


Sehemu ya Ujumbe wa Benki ya Dunia ikiwa kwenye kikao.

Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania (juu na picha mbili chini) wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri kwenye kikao hicho.






Ujumbe wa Benki ya Dunia na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja.
(Picha na Mhariri wa Habari hii ni FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni