Ijumaa, 16 Agosti 2024

MAHAKAMA ZA MWANZO TANO KUJENGWA KANDA YA DAR ES SALAAM

Na TAWANI SALUM-Mahakama-Dar es Salaam

Ujenzi wa Mahakama za Mwanzo tano katika Kanda ya Dar es Salaam unatarajia kuanza wiki ijayo tarehe 22 Agosti, 2024.

Hatua hiyo inafuata baada ya Mahakama kukabidhi maeneo ya ujenzi kwa Mkandarasi atakayetekeleza mradi huo.

Mahakama hizo ni Mahakama ya Mwanzo Mbagala na Somangila katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mahakama ya Mwanzo Kimanzichana, Bungu na Msata katika Mkoa wa Pwani.

Jana tarehe 15 Agosti, 2024, Kampuni ya Ujenzi ya Deep inayoongozwa na Bw. Rabinder  Jabbal walikutana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi kukabidiana rasmi mradi huo.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Mhe. Maghimbi alisema kuwa ujenzi wa Mahakama hizo tano utaleta kichocheo cha maendeleo kwa kuwa wananchi hawatakwenda umbali mrefu kutafuta haki.

‘’Nataka tukutane tena hapa kukiwa na habari njema ya kumaliza ujenzi wa Mahakama hizi zilizopo ndani ya Kanda ya Dar es Salaam, ni imani yangu mradi huu utamalizika kama tulivyokubaliana. Kila upande ufanye kazi yake kama mkataba unavyosema ili kutimiza malengo ya Mahakama ya Tanzania pamoja na Taifa letu kwa ujumla,’’ alisisitiza Jaji Maghimbi.

Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Ujenzi ya Deep alisema kuwa mradi huo ambao utachukua miezi sita kuanzia tarehe 22 Agosti,2024 utamalizika kwa wakati kama mkataba unavyosema kwa kuwa kila kitu kipo sawa na kinachosubiriwa ni kufika kwa tarehe husika ili kuanza ujenzi.

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka alisema kuwa ujenzi wa Mahakama hizo utakuwa ni kichecheo cha upatikanaji wa haki kwa haraka na wakati, hivyo basi kutimiza dhima na dira ya Mahakama ya Tanzania.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakam Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Livin Lyakinana alimshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa Mahakama ya Tanzania.

Gharama za mradi huo ni Shilingi za Kitanzania zipatazo 3,996,465,350/- ambazo Serikali ya Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania imezitoa na kuipa Mahakama ya Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hizo.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Moses Mashaka (kushoto) na Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Livin Lyakinana (kulia) wakiwa katika kikao cha makabidhiano ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Mahakaama za Mwanzo tano.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akiwa na wadau wengine kwenye kikao hicho.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni