Jumamosi, 17 Agosti 2024

MAHAKIMU PWANI WAKUMBUSHWA KUZINGATIA MIONGOZO YA KAZI

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amewakumbusha Mahakimu kuzingatia miongozo mbalimbali ya kazi na maelekezo ya Viongozi ili kuongeza ufanisi  na kuleta tija kwenye kazi ya utoaji haki.

Mhe. Maghimbi aliyasema hayo tarehe 16 Agosti, 2024 katika ukumbi wa Ruvu JKT Kibaha mkoani Pwani alipokuwa akifungua mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT) Pwani.

“Ni jukumu la kila Mfawidhi kuhakikisha anaimarisha maadili ya watumishi walio chini yake katika kituo chake kwakuwa kila mtu anajua kazi tunayofanya ni nyeti na inahitajika kufanyika kwa uadilifu mkubwa kwa kufuata msingi ya kisheria ya haki na kutafsiri sheria,” alisema Mhe. Jaji Maghimbi.

Kadhalika Mhe. Maghimbi amewakumbusha Wafawidhi hao kukemea bila woga wanaoonekana kupotoka  aidha kwa kuonekana ni watovu wa nidhamu au hawazingatii maadili. 

Aliongeza kuwa, uwajibikaji na nidhamu kazini vinaimarisha zaidi uhuru wa Mahakama na taswira ya Mahakama kwa jamii na kwa wote wanaohitaji huduma kutoka katika Mhimili huo.

“Haya yakifanyika itachukuliwa fahari kwa chama cha Majaji na Mahakimu kwa kuwa kazi yake pia ni kusimamia maadili na utendaji na kukumbushana miongozo mbalimbali,” alisisitiza.

Kadhalika, Mhe. Maghimbi hakusita kukumbusha kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

“Mfumo wa Sheria na Mahakama umeendelea kukua na kubadilika kadri jamii inavyobadilika na tumeona Mahakama ikilazimika kuboresha uendeshaji wa shughuli zake kwa kuingia katika mfumo wa TEHAMA hivyo basi ni jukumu lenu nyinyi kama Mahakimu kuhakikisha JMAT inaona Fahari kuwatumikia na kuwasimamia kwa kuhakikisha kua hamko nyuma katika maswala ya TEHAMA” alisema Mhe. Maghimbi.

Aidha, Mhe. Maghimbi aliwaomba Mahakimu hao kujifunza bila kuchoka kujua mtandao ambapo alisema hatamuelewa Hakimu yoyote atakayefungua jalada gumu badala ya mtandao.

“Inabidi kuuzoea, kuupenda na kuutumia mfumo kwa maslahi mapana ya Mahakama ya Tanzania kwani Mahakama haitegemei kurudi nyuma kwenye matumizi ya nyaraka ngumu hivyo mtake msitake mgeni kaja katua mzigo yupo haondoki hivyo tengenezeni chumba naye awe sehemu ya familia haondoki tena,” alieleza Jaji Maghimbi. 

Ameongeza kwamba, kuuchukia mfumo huo ni kujitesa na kujisababishia matatizo katika kazi kwa kuonekana mzembe na kutofuata maelekezo ya Viongozi na kusema kuwa hali hiyo inaweza kusababisha mhusika kufikishwa kwenye kamati za maadili.

Kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti ambaye pia ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi.

Dhumuni la kikao hicho ni kujadili na kupitia changamoto wanazokabiliana nazo wakati wa utendaji kazi hasa kupitia mfumo wa usikilizaji mashauri kwa Mahakama za Wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi vilevile Mfumo wa Kusajili Mashauri katika Mahakama za Mwanzo.

Katika hafla hiyo mwenyekiti wa chama cha Majaji na Mahakimu Pwani Mhe. Joyce Mkhoi aliwashukuru kwa ushirikiano  katika kazi  kipindi wako Pwani na upendo waliouonyesha.

Baada ya kikao hicho kulifanyika pia hafla fupi ya kuwaaga baadhi wa Mahakimu waliohama Mkoa wa Pwani na kuhamia sehemu mbalimbali.

Naye Mwakilishi wa waagwa hao ambaye ni Hakimu Mkazi, Mhe. Nabwike Mbaba aliwashukuru Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Pwani kwa ushirikiano waliouonesha kipindi walipokuwa pamoja na ameahidi watapeleka upendo huo huko walipo. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akiwa katika picha na Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT) Pwani mara baada ya kikao cha Chama hicho mkoani humo tarehe 16 Agosti, 2024 katika ukumbi wa Ruvu JKT Kibaha.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Mary Moyo na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi mara baada ya kufungua kikao cha Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT) Pwani.

 
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akiwa katika picha ya pamoja na wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT) Pwani baada ya ufunguzi wa kikao.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akiweka saini kwenye kitabu cha wageni alipowasili katika ukumbi wa Klabu ya Ruvu JKT Kibaha mkoani Pwani kwa ajili ya kufungua kikao cha Chama cha Majaji na Mahakimu mkoani humo.

Wanachama wa JMAT waliohama Pwani wakikata keki ya upendo kwa ajili ya kuwaaga katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa JKT Ruvu Kibaha mkoani Pwani.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni